FUNGUO ZA KUNG'ATUKA:Siyo kwa nguvu kuchoka, mwenyewe aliwajibika

NA LWAGA MWAMBANDE

HAYATI Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule ilikuwa Tanganyika).

Oktoba 14, 1999, ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe kwani Mwalimu Nyerere aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St.Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua kansa ya damu.

Mwili wa Mwalimu ulipokelewa jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani jijini humo.

Oktoba 20, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao.

Aidha,Oktoba 21, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria ibada hiyo. Watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi Oktoba 22, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya maziko.

Maziko ya Mwalimu Nyerere yalifanyika Oktoba 23, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika Kijiji cha Butiama, wilayani Musoma Vijijini, mkoani Mara.

Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alikua akiamini katika falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,Baba wa Taifa wakati wa uhai wake alitenda mengi kwa mustakabali na maslahi mapana ya Taifa, ndiyo maana alikuwa akitumia maarifa, hekima na busara kufanya maamuzi bora kwa ustawi mwema wa jamii ya Watanzania na Taifa kwa ujumla, endelea hapa chini;

1:Wazo limeshanifika, Nyerere alivyoondoka,
Kimoja aling'atuka, bila ya kulazimika,
Siyo kwa nguvu kuchoka, mwenyewe liwajibika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

2:Shida sana kung'atuka, umri unapofika,
Ni kuzidi teulika, na hata kuchagulika,
Vijana wasikitika, ajira zinafinyika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

3:Ajira kaajirika, sitini imeshafika,
Pensheni kwake yalika, lakini hajaridhika,
Tena anateulika, husikii akimaka,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

4:Mzee kateulika, ajira anatumika,
Tena huyo asikika, vijana akiwataka,
Wasingoje ajirika, eti kazi mefutika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

5:Nyerere twamkumbuka, yake mengi yasomeka,
Ni mwenyewe alitaka, kuachia madaraka,
Nani leo anataka, mwenyewe akang'atuka,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

6:Chaguzi zinafanyika, hapa kwetu Afrika,
Figisu ni takataka, pande zote kigeuka,
Usitake unataka, wapo wa kuchagulika,
Mbinu zote zatumika,Hatamu kuzidi shika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

7:Wengine waliposhika hatamu wanazeeka,
Hawataki kuondoka, mpini wamaushika,
Makali kitaka shika, maumivu yatafika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

8:Vigezo alivyoweka, ni vigumu kufikika,
Si mali kutakataka, jinsi alivyoridhika,
Yale mambo kuhongeka, kwake hayakusikika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

9:Jambo la kusikitika, Mwalimu kumkumbuka,
Hata wasiohusika, heshima wambandika,
Huku yanayofanyika, likwishasahaulika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

10:Mwalimu wa kutukuka, utajiri hakutaka,
Bali watu kuinuka, waweze kuelimika,
Madaraka weze shika, na kazi kuchakarika,
Funguo za kung'atuka, mfukoni aliweka.

Lwaga Mwambande (KIMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news