Rais Samia kufanya ziara siku nne mkoani Kigoma

NA RESPICE SWETU

WAKAZI na wananchi wa Mkoa wa Kigoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumlaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake ya siku nne anayotarajia kuifanya mkoani humo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu ugeni huo.

PICHA NA IKULU.

Amesema kuwa, kufanyika kwa ziara hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuwa katika ziara hiyo, Rais Samia pamoja na kuzungumza na wananchi, ataweka mawe ya msingi, atazindua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Hii ni ziara ya kwanza tangu Rais Samia aingie madarakani, hivyo ni faraja kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kutembelewa na Mheshimiwa Rais, nachukua nafasi hii kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Kigoma kumlaki na kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote atakayopita,”amesema.

Akizungumzia ratiba ya ziara ya Mheshimiwa Rais Andengenye amesema, Rais Samia Hassan Suluhu atapokelewa mkoani Kigoma Jumapili Oktoba 16, 2022 majira ya saa 4 asubuhi katika Wilaya ya Kakonko na kuendelelea na ziara kwenye wilaya zote za mkoa wa Kigoma hadi Oktoba 19 atakapokamilisha ziara hiyo.

Miongoni mwa miradi itakayotembelewa na Mheshimiwa Rais katika siku nne za ziara yake mkoani Kigoma ni miradi ya elimu, barabara, afya na maji pamoja na kuzungumza na wananchi.

Post a Comment

0 Comments