MADARAJA UDHIBITI-2:Mkeo, watoto na ndugu zako unawaacha katika hali gani?

NA LWAGA MWAMBANDE

KILA siku ajali za barabarani hukatili uhai wa maelfu ya watu ndani na nje ya Tanzania, ni ajali hizo hizo ndizo ambazo zimekuwa zikiwaacha watu na ulemavu wa kudumu katika maisha yao.

Vivyo hivyo, kuleta maumivu katika familia nyingi ambazo huwa zinapoteza wapendwa wao, ambao huwa wanawategemea katika mahitaji yao ya kila siku.

Ni wazi kuwa, Tanzania bila ajali inawezekana, kuwezekana huko kunatokana na uamuzi wa kila mmoja wetu iwe dereva, anayeendeshwa au abiria kuamua kwa dhati kabisa kuwa, hata bila mwendokasi au kwa namna yoyote ile inawezekana kufika au kurudi salama kokote huendako.

Credit:bressmanlaw.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema mustakabali wa familia nyingi kutokuwa na vifo, walemavu wanaotokana na ajali umebebwa na dereva anayeendesha chombo cha moto barabarani. Jiulize ukifa leo kwa ajali malengo uliyojiwekea maishani, ile familia yako akiwemo mkeo, watoto na ndugu zako unawaacha katika hali gani? Endelea;

1:Madaraja udhibiti, bora hayo kuyaweka,
Kote tuweze dhibiti, ajali zitatoweka,
anuni ziwe thabiti, tena za kueleweka,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

2:Binafsi inatosha, alama mmeziweka,
Magari wakiendesha, ni rahisi kuwashika,
Ikibidi kuwatisha, adhabu zikiwafika,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

3:Kwa hali ilivyo sasa, alama zinatumika,
Siyo kwa wenye msasa, jinsi huko zavunjika,
Bali kwa raia hasa, ambao waeleweka,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

4:Kama spidi sabini, binafsi ile afika,
Mia moja thelathini, wa umma ataridhika,
Hapo kuwe umakini, waweze kudhibitika,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

5:Kupita gari kwa kona, kwa wengi yaeleweka,
Ajali unaiona, kwamba yaweza kufika,
Lakini wengine ona, akatisha anafika,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

6:Wao iwe mara mbili, yawapasayo kushika,
Hapo na tuwe wakali, ajali kudhibitika,
Vinginevyo tumefeli, vifo tazidi tufika,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

7:Wao wanavyokimbia, mdomo waweza shika,
Wasemapo subiria, kwao hapo papitika,
Kizuia kuingia, hapo panaingilika,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

8:Sasa anapokatisha, kiongozi abebeka,
Pale akikinukisha, na kifo kikamfika,
Ndipo tutajionesha, hilo linaeleweka?
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

9:Kwa ajali tutanuka, bila hatua kushika,
Vifo tazidi tufika, hata vya kuzuilika,
Kombe tunavyofunika, mwanaharamu acheka,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

10:Akili zetu zaona, moyoni twasikitika,
Twajua hatutapona, hatari tazotufika,
Kusema siye twanuna, kutanua kwatanuna,
Kuwe mlango wa umma, na ule wa binafsi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news