Majaliwa ahimiza mshikamano kuijenga CCM,ataja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa Awamu ya Sita

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wana-Ruangwa waendelee kushikamana ili kukijenga Chama cha Mapinduzi (CCM) na kukifanya kibaki kuwa na nguvu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa akipiga kura ya kumchagua Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Ruangwa katika Mkutano Mkuu wa CCM wilaya ya Ruangwa wa kuchagua viongozi wa CCM wa wilaya hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Awali na Msingi Wonder Kids ya Rungwa, Oktoba 2, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Nasisitiza haya kwa sababu hata Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametaka wanachama tushikamane tujenge upendo miongoni mwetu na tusimamie chama chetu ili kiwe na nguvu katika maeneo yetu,” amesema.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa ametoa wito huo leo Jumapili, Oktoba 2, 2022 wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wilayani Ruangwa kutoka kata 22 uliofanyika ili kuwachagua viongozi wa wilaya hiyo.

“Kama eneo la Ruangwa litakuwa na nguvu, Nachingwea litakuwa na nguvu, Liwale litakuwa na nguvu, Kilwa litakuwa na nguvu, Lindi Vijijini na Manispaa yatakuwa na nguvu, mkoa wa Lindi automatically utakuwa na nguvu kisiasa na mimi naamini Ruangwa hatutamwangusha Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.” Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa akiweka kura yake kwenye sanduku la kura katika Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ruangwa wa kuchagua viongoziwa CCM wa wilaya hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Awali na Msingi Wonder kids, Ruangwa Oktoba 2, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo mafanikio yaliyopatikana wilayani humo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo ujenzi wa shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, miradi ya maji, chuo cha VETA, mabweni ya wanafunzi wa sekondari, maji na umeme.

“Sisi wilaya ya Ruangwa tumetekeleza vizuri Ilani ya CCM na Rais Samia ametuunga mkono sana. Nani hajui kama wilaya hii ilikuwa na upungufu mkubwa kwenye sekta ya elimu? Nani hajui kwamba hatukuwa na shule za msingi katika kila kijiji? Lakini leo tumejitahidi na tumefikia zaidi ya asilimia 90. Ahadi ni kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2025, kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi,” amesisitiza.

Akifafanua zaidi kuhusu elimu, Mheshimiwa Majaliwa amesema kulikuwa na kata tatu za Mbwemkuru, Nandagala na Nanganga ambazo zilikuwa hazina shule za sekondari lakini hivi sasa kila kata imepewa sh. milioni 470 na ujenzi umeshaanza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ruangwa wa kuchagua viongozi wa CCM wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa Shule ya Awali na Msingi, Wonder Kids iliyopo Ruangwa, Oktoba 2, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Pia tumepewa shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule maalumu ya wasichana watakaochukua masomo ya sayansi. Shule hii iko Ruangwa, nyuma ya uwanja wa mpira wa Majaliwa na itaanza kufundisha kuanzia Januari, 2023.”

Amezitaja shule nyingine zilizojengwa kuwa ni ya Kitandi ambayo pia itaanza kufundisha kuanzia Januari, 2023. “Wilaya hii, watoto wetu wa kike bado wana changamoto nyingi, kwa vile Liugulu kuna sekondari mbili, tumeamua moja iwe na wavulana na nyingine iwe ya wasichana na zote hizi tunazijengea mabweni ili vijana wetu wapate malezi mazuri shuleni.”

Amesema wilaya hiyo ilipokea sh. bilioni mbili za ujenzi wa Chuo cha VETA na kuwaarifu wajumbe hao kwamba wamepata eneo la ekari 70 na ujenzi wake umekamilika isipokuwa wanasubiri kuingiza maji.

Kuhusu afya, Mheshimiwa Majaliwa amewaeleza wajumbe hao kuwa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo imefikia hatua nzuri na vituo vya afya vya Luchelegwa, Nandagala, Ruangwa, Narung’ombe, Nangurugai, Namichiga na Mandawa umekamilika. “Itabakia kata moja ya Nambilanje,” amesema.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa CCM wa wilaya ya Ruangwa wa kuchagua viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wakimsikiliza Waziri Mkuu na Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa wakatika alipozungumza kwenye ukumbi wa Shule ya Awali na Msingi, Wonder Kids iliyopo Ruangwa, Oktoba 2, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kuhusu umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema kazi ya kusambaza umeme vijijini inaendelea na lengo la wilaya ni kuhakikisha ifikapo Desemba 2022, vijiji vyote viwe vimepata umeme.

Uchaguzi bado unaendelea wa kuwachagua Mweyekiti wa CCM wa Wilaya, Wajumbe watatu wa Mkutano Mkuu Taifa, Wajumbe 10 wa Halmashauri Kuu ya Wilaya na Wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu ya Mkoa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news