Makamu wa Kwanza wa Rais asema utafiti ni silaha kubwa ya kupambana na Ukimwi

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema, Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania ni muhimu katika kuiwezesha Serikali na wadau mbalimbali kupata picha halisi ya mwenendo wa maradhi hayo na kusaidia kuweka mikakati ya kwenda sambamba na uhalisia katika kupambana na tatizo hilo.
Mhe. Othman ameyasema hayo leo huko hoteli ya Verde Mtoni-Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakati akizungumza katika uzinduzi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi nchini unaotarajiwa kufanyika Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema kwamba, kupatikana kwa takwimu sahihi ni silaha muhimu katika kupanga na kuaandaa mikakati ya kupambana na maradhi hayo kwa kuwa itasaidia kufahamika mwenendo wa tatizo hilo kwa ukamilifu.
Hata hivyo, Mhe. Othman amesema kwamba kwa upande wa Zanzibar ni vyema utafiti huo kwenda sambamba na kwa kuhusisha makundi maalum ambayo yanaaminiwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya maradhi hayo ikilinganishwa na jamii ya kawaida.

Aidha, amebainisha kwamba utafiti huo utahusisha kaya zipatazo 20,000 kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kuwataka wananchi kuondoa hofu juu ya suala hilo na kuona kwamba kaya zote zina fursa sawa ya kushiriki kwenye utafiti huo.
“Kwa ujumla inatarajiwa kwamba utafiti huu wa mwaka 2022/2023 utahusisha watu wapatao 40,000,ni matumaini ya Serikali kwamba kaya zilizochaguliwa na watu watakaohusika watatoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha suala hilo muhimu na kwamba taarifa zitakazopatikana zitaendelea kuwa siri na zitatumika kitakwimu pekee,”amesisitiza Makamu huyo wa Rais.

Mhe.Othman amesema, Tanzanzia inayo mikakati kadhaa ya kupambamba na tatizo hilo kwa kuwa ni muhimu pia katika kusaidia nchi kupiga hatua kiuchumi na kuilinda nguvu kazi yake.
“Ugonjwa wa Ukimwi umeshapoteza idadi kubwa ya watu Duniani, kama nchi tumefurahia fursa hii ya utafiti kwani itasaidia sana katika kuboresha zaidi mikakati yetu ya kupambana na gonjwa hili sambamba na kuilinda nguvu kazi yetu,”amesema.
Mhe. Othman ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia kituo chake cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa kwa kuendelea kuisaidia nchi kitaalamu na kifedha kuweza kufanya utafiti huo muhimu katika kupambana na maradhi ya Ukimwi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Harusi Said Suleiman amesema katika kuyafikia malengo ya kuondosha maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi hakuna budi kupata utafiti wa kitaalamu ili kuona namna bora ya kupambana.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Mhe. Suzan Peter Kunambi amesema, matumizi ya dawa za kulevya na biashara za ngono ni miongoni mwa mambo yanayosababisha idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, hivyo uwepo wa tafiti kutasaidia kujua idadi na kudhibiti tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, Dkt. Ahmed Khatib, amesema kwamba Zanzibar kumekuwa na mikakati mbalimbali ambayo imesaidia sana katika kupambana na kudhibiti ugonjwa huo tokea alipobainika mgonjwa wa kwanza mnamo mwaka 1986 hapa Zanzibar.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Salim Kassim Ali amesema, kwamba utafiti huo utawahusisha watu kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea, na kwamba takwimu zitakazopatikana zitasaidia sana katika kubuni sera mpya na kusaidia serikali katika kupanga mikakati zaidi ya kupambana na ugonjwa huo.
Utafiti huo unasimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Zanzibar (ZAC), Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Wizara ya Afya Tanzania Bara na Zanzibar, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine wa sekta mbalimbali.

Katika ufunguzi wa utafiti huo, shughuli mbalimbali zimehusika ambazo ni pamoja na kutembelea mabanda ya maonesho, taarabu asilia na maigizo.
Viongozi mbalimbali wa Kiserikali, siasa, dini na mabalozi wamehudhuria katika shughuli hiyo akiwemo Bw. Robert Raines ambaye ni Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania), Dkt. Mahesh Maruyama (Mkurugenzi wa ICAP Tanzania), Bi. Daima Mohamed Mkalimoto (Mkurugenzi wa Mipango na Uendeshaji Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar) na Bw. Salim Abdallah Bimani (Kaimu Naibu Katibu Mkuu ACT Wazalendo Zanzibar).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news