Mama Mariam Mwinyi asisitiza wanawake kuwatii waume zao

NA DIRAMAKINI

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi amesisitiza umuhimu wa wanawake wa Kiislamu nchini kuwatii waume zao pamoja na kutekeleza haki zao katika mambo yalioelekezwa na Mwenyezi Mungu.
Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi (wa pili kushoto) akikaribishwa na akinamama wa Madrasatul Mushawar Mwembeshauri katika Maulid ya kumsifu Mtume Muhamad S.A.W yaliyosomwa leo katika masjid Mushawar Mwembeshauri Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi. (Picha na Ikulu).

Mama Mariam ameeleza hayo katika nasaha alizotowa kwa wanawake wa Kiislamu walioshiriki katika Maulid ya kumswalia Mtume Muhammad (SAW) yaliofanyika katika Msikiti wa Muembeshauri, Mkoa Mjini Magharibi.

Maulid hiyo imeaandaliwa na Jumuiya ya Wanawake wa Msikiti wa Mwembeshauri, ambapo imewashirikisha waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Amesema, kuna umuhimu mkubwa kwa akinamama wa kislamu kuwatii waume zao katika kutekeleza mambo mema, na akatumia fursa hiyo kumuomba Mwenyezi Mungu kuizidishia utiifu jamii hiyo.

Aidha,Mama Mariam amekubali maombi ya kuwa Mlezi wa jumuiya hiyo pamoja na kusaidia harakati za kuiendeleza katika kufanikisha ujenzi wa jengo lake, sambamba na msaada wa huduma za kujikumu kwa wageni waliotoka Mtwara ambao watakuwepo Zanzibar kwa kipindi cha wiki moja.
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi (wa pili kushoto) akiitikia dua ya Ufunguzi wa Maulid ya kumsifu Mtume Muhamad S.A.W iliyosomwa na Bi.Asha na Bi.Uchungu (wa Pili kulia) katika Masjid Mushawall Mwembeshauri Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi leo,ambayo imeandaliwa na Madrasatul Mushawar Mwembeshauri.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Fatma Mliwa akitoa mawaidha katika Maulid hayo amesema uzawa wa Mtume Muhammad (saw) ni fadhila na rehemu kubwa kutoka Mwenyezi Mungu, kwani amekuja kubainisha mazuri na mabaya.

Aidha, Bi.Ashura kutoka Mtwara akitoa salamu za akinama kutoka Mtwara aliishukuru jumjuiya hiyo ya akinamama wa Msikiti wa Muembe Sahuri kwa mwaliko walioupata na katumia fursa hiyo kuondosha dhana kuwa Maulid ni Bidaa na hivyo akasisitiza umuhimu wa kumsifia Mtume.
Mapema, akitoa mawaidha katika maulid hayo,Bi.Mkubwa Omar alisitiza umuhimu wa akinamama wa kiislamu kuwatii na kutekeleza haki za waume zao, huku akibainisha mambo mbalimbali wanayopaswa kutekeleza ikiwemo la kutotoka nyumbani bila ridhaa za waume zao pamoja na kudai talaka bila sababu zozote za msingi.

Post a Comment

0 Comments