Mhe.Othman:Tuwaenzi wazee ili kulivusha Taifa

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza haja ya kuwaenzi na kuwathamini wazee, kuwa ni mwendelezo wa utamaduni uliowachwa na viongozi waliopigania ukombozi wa nchi, ili kujenga ustawi bora wa jamii.
Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, ameyasema hayo leo, kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wazee pamoja na familia mbalimbali alizotembelea katika ziara yake maalum visiwani hapa.
Amesema kuwa Wazee ni hazina kubwa inayostahiki kuenziwa, kwani kuwepo kwao kunaashiria pia uwepo wa muendelezo wa hikma, mila, silka, malezi na jamii inayoendelea kulelewa kwa misingi ya maadili kupitia kizazi kimoja kwenda chengine.
“Nasi tunaendelea kujisikia faraja kwa kuona wazee wetu bado mpo; hatunabudi kuendeleza utamaduni wetu wa kupendana na kusaidiana ikiwemo kutembeleana, kwa watu wote, pamoja na wale wenye changamoto mbali mbali,"ameeleza Mheshimiwa Othman.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Othman amewatembelea pia Maalim Abdulrahman Bakar Omar ‘Maalim Abouf’, Maalim Suleiman Mohamed Suleiman ‘Babu Sule’ wa Michenzani; Familia ya Bi Amina Awesu; Mzee Talib Kassim wa Monduli; na Msomi-Mwanasiasa mashuhuri hapa Nchini, Dokta Juma Ameir Muchi, huko Mwanakwerekwe, pia Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.
Miongoni mwa Wazee waliotembelewa katika ziara hiyo, Mzee Hamad Salim (79) Mkaazi wa Magomeni Kwa-Najim, ametoa wito kwa Viongozi wa Serikali na Vyama Siasa kuendelea kuijali rika na sehemu hiyo muhimu ya jamii.

Amesema kuwa, wazee wa hapa visiwani wameutumia umri wao mwingi katika kupigania Mamlaka ya Nchi bila ya kukata tamaa, hivyo ni wajibu wa viongozi waliopo madarakani sasa, kuendeleza jukumu hilo “kwa kuendelea kutweka tanga hadi pale jahazi litakapofika ufukweni kwa salama na mafanikio zaidi”.
Masheha na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, na Vyama vya Siasa, akiwemo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Bw. Salim Bimani, wameambatana na Mheshimiwa Othman, katika ziara hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news