Michezo ya SHIMIWI inajenga afya-Waziri Mhagama

NA VERONICA MWAFISI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) inasaidia kujenga afya za watumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao vema na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akicheza netiboli katika uwanja wa Bandari jijini Tanga wakati wa Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI).
Baadhi ya washiriki wa Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akifungua Sherehe za Michezo hiyo katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Mhe. Jenista amesema hayo, wakati akifungua rasmi Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) kwa mwaka 2022 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, iliyoanza Oktoba 1, 2022 na inatarajiwa kufikia tamati Oktoba 15, 2022.
Mhe. Jenista amesema, Serikali inaendeleza michezo ya SHIMIWI ili kujenga afya za watumishi wa umma nchini na kuhakikisha inakuwa na rasilimaliwatu yenye tija katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ameongeza kuwa, kutokana na umuhimu wa michezo ya SHIMIWI, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alielekeza kurejeshwa kwa michezo ya SHIMIWI ili itumike kujenga afya ya akili na mwili kwa watumishi wa umma nchini, maelekezo ambayo yalitolewa na Mhe. Waziri Mkuu wakati akimuwakilisha Mhe. Rais Samia kwenye mbio za hisani zilizoandaliwa na benki ya CRDB.
Aidha, Mhe. Jenista awewataka watumishi wote wa umma wanaoshiriki michezo ya SHIMIWI mwaka huu, kuzingatia nidhamu na uadilifu katika kipindi chote watakachokuwa jijini Tanga wakishiriki michezo hiyo ya SHIMIWI.

“Sitegemei kusikia kuna mtumishi yeyote amejihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu kwani michezo ya SHIMIWI ni sehemu ya kazi,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Wizara ya utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amewapongeza watumishi wote waliopo jijini Tanga kuziwakilisha taasisi zao na kuwataka kuzingatia nidhamu katika kipindi chote wanachoshiriki michezo ya SHIMIWI.

“Ni matumaini yangu kuwa, michezo hii itaendeshwa kwa kuzingatia nidhamu, weledi na viwango vya hali ya juu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali,” Mhe. Gekul amesisitiza.
Mhe. Gekul ameongeza kuwa, licha ya michezo hiyo kujenga afya za watumishi wa umma pia inasaidia kujenga undugu, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa umma na hatimaye kuweka mazingira mazuri ya kufikia lengo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kuujenga utumishi wa umma wenye kuzingatia uadilifu na uwajibikaji.

Naye, Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa watumishi wa umma na kuridhia watumishi wa sekta zote kushiriki michezo ya SHIMIWI kwa ajili ya kujenga afya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mchezo wa netiboli kabla ya kuanza kwa mchezo huo katika uwanja wa Bandari jijini Tanga wakati wa Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI). Watatu kutoka kulia ni Naibu Waziri, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul na watatu kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Bw. Omary Mgumba.

Sanjari na hilo, Bw. Mwalusamba, amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kwa kufungua michezo hiyo muhimu inayowakutanisha watumishi wa umma kutoka katika Wizara, Mikoa, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali ambao wananufaika na michezo katika kujenga afya zao.

Zaidi ya watumishi 1000 wanashiriki michezo ya SHIMIWI mwaka huu inayojumuisha soka, netiboli, riadha, kuvuta kamba, bao, kurusha tufe, karata, mbio za baiskeli pamoja na drafti na yenye Kaulimbiu “Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na huongeza tija mahala pa kazi…..Kazi Iendelee”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news