Waziri Mhagama atoa maagizo kwa wajumbe Baraza Kuu la Wafanyakazi

NA JAMES K.MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka wajumbe wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara kuhakikisha wanashughulikia kwa wakati malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika maeneo yako ya kazi kama serikali ilivyokusudia, ili kuwapunguzia gharama za kusafiri hadi Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa masuala yao ya kiutumishi.

Wajumbe wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akifungua mkutano wa baraza hilo mjini Morogoro.

Mhe. Jenista ametoa wito huo kwa wajumbe wa baraza hilo, wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara unaofanyika mjini Morogoro.

“Wajumbe wa baraza, mnaposhughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi mhakikishe mnayashughulikia kwa wakati ili kuwaondolea mzigo wa gharama katika kutafuta ufumbuzi kwa viongozi na waajiri kwenye ngazi ya kitaifa,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikisisitiza umuhimu wa watendaji kushughulikia malalamiko ya watumishi wa umma ili kuwajengea ari na morali ya kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo wajumbe wa baraza hawana budi kuunga mkono jitihada za serikali kuhimiza ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma nchini.

Katika kutoa msisitizo wa ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi na watumishi wa umma, Mhe. Jenista ametoa wito kwa waajiri kuutumia ipasavyo mfumo wa e-Mrejesho katika kushughulikia malalamiko ili kupata mrejesho utakaotumiwa na serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Bi. Jane Mihanji amesema, baraza litatoa kipaumbele cha matumizi ya e-Mrejesho serikalini ili kuendana na kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo inakua kwa kasi kubwa.

Akizungumzia uwajibikaji kwa wajumbe wa baraza, Bi. Mihanji amesema kuwa wao kama viongozi na wawakilishi wa watumishi wa umma watahakikisha wanawakumbusha watumishi kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ili wawe na uhalali wa kudai haki na stahili zao pindi wanapozikosa kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema wajumbe wa baraza watashiriki katika kutekeleza ajenda kuu moja ya msingi ya kupitia na kuridhia miundo ya maendeleo ya utumishi ya kada zilizo chini ya wizara mbalimbali katika Utumishi wa Umma ili kuendana na mahitaji ya watumishi wa umma nchini.

Mkutano huo unaoratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, unafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 06 hadi 8 Oktoba, 2022.

Post a Comment

0 Comments