Mikoa 17 kukosa umeme Jumapili hii na Jumatatu

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) leo Oktoba 8, 2022 limetoa taarifa ya kukosekana kwa umeme kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, TANESCO Makao Makuu ambayo imefafanua kuwa, baadhi ya maeneo yatakosa umeme kwa siku ya Jumapili ya Oktoba 9 na Jumatatu ya Oktoba 10, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo baadhi ya maeneo yatakayoathirika ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha, Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Shinyanga, Tabora, Mwanza, Mara, Simiyu, Kilimanjaro, Manyara na Songwe.

"Sababu za katizo hilo la umeme ni kuzimwa kwa laini mbili kubwa za umeme wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Kinyerezi na kutoka Morogoro hadi Kidatu ili kuruhusu matengenezo ya uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji umeme katika Kituo cha Msamvu, Morogoro,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katizo la umeme Jumapili ya Oktoba 9, 2022 litaanza kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 10:30 jioni huku Jumatatu ya Oktoba 10, 2022 itaanzia saa 1:30 hadi saa 9:30 alasiri.

Post a Comment

0 Comments