Serikali yatoa maagizo kwa kampuni za simu

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Nnauye ameziagiza kampuni za mawasiliano ya simu nchini kuanzisha huduma maalumu kwa ajili ya vikundi vya wajasiriamali wadogo wanawake ili viweze kufanya kwa urahisi na kwa gharama nafuu biashara kwa njia ya kidigitali.

Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa Waziri Nape ametoa siku 14 kuanzia leo Oktoba 8, 2022 Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kukutana na kampuni hizo za utoaji wa Huduma za Mawasilino ili kuweka mfumo huo na kuagiza kwamba mbali na kuuweka, lakini pia uwe wa gharama nafuu.
Waziri Nape ametoa agizo hilo leo, wakati akihutubia baada ya kufungua Maonesho ya Kongamano la Women of Hpe Alive (WHA) la Wanawake Wajasiriamali, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Kongamano,ambalo limehudhuriwa na wanawake zaidi ya 6,000 kutoka vikundi mbalimbali vya wanawake wajasiriamali wadogo na wakati vilivyopo chini ya usaidizi wa WHA.

Waziri Nape ametoa agizo hilo, akijibu moja ya maombi yaliyotajwa na WHA katika risala iliyosomwa kwake na Katibu wa WHA, Saumu Mbwana, wakati wa hafla hiyo ambapo aliomba kampuni za simu kupitia TCRA ziweke huduma rafiki itakayowawesha wajasiliamali wadogo na wakati Wanawake kuweza kufanya mawasiliano ya biashara kidigitali kwa urahisi na bei nafuu.

"Zipo huduma za Wapenzi, Michezo nakadhalika zinazotolewa na Kampuni za Simu, sasa mimi sioni kama kuna ugumu wowote kwa kampuni hizi kuanzisha huduma hii kwa Wanawake Wajasiriamali wa WHA, ili muweze kufanya shughuli zetu za kibiashara kidigitali kama mlivyodhamiria.

"Hivyo kwa kuwa jambo hili linawezekana, naiagiza TCRA kukutana na Kampuni hizi zote za simu ndani ya siku 14 ili kuweka huduma hii mara moja,"amesema.

Waziri Nape aliwapongeza WHA kwa kuja na wazo la kuingia katika Uchumi wa Kidigitali, akisema ni wazo zuri sana kwa kuwa wamekuja nalo katika wakati muafaka, kwa sababu ndivyo dunia sasa inavyotaka maaba imefikia wakati ambapo inawezekana kufanya biashara kwa njia ya mtandao.

Alimpongeza Mwanzilishi wa WHA, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga kwa kuja na kufanikisha wazo wa kuwakusanya Wanawake Wajasiliamali hasa wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuwa hilo siyo jambo rahisi hasa wa mtu ambaye ni mara ya kwanza kuwa Mbunge.

"Mimi najaua ikiwa ndiyo mara ya kwanza mtu kuwa Mbunge wengi huhangaika kwanza kutafuta apitie wapi ili kuja na wazo lenye tija na likafanikiwa. Hili alilofanya ni jambo kubwa sana kwake, kwa maana nyingine ni sawa na mtoti aliyezaliwa akiwa mkubwa,"amesema.

Awali Mbunge Janeth Mahawanga alisema, hilo ni kongamano la nne kufanyika tangu WHA ilipoanzishwa mwaka 2012 na katika jitihada za kuliboresha safari hii wameamua liambatane na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali za wanawake ili wanawake hao chini ya WHA wapate fursa za kutangaza na kuuza bidhaa na huduma hizo.

Mbunge huyo amewataka wanawake kupitia WHA kuimarika kama moja ya njia ya kuuga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwainua kimaisha wanawake wote hapa nchini, kwa kuwa tofauti na mwanzo ambapo kikwazo kikubwa ilikuwa mikopo, sasa kikwazo hizo hakipo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news