Serikali yatumia Bilioni 1/- kuboresha Chuo cha Ualimu Butimba

NA MATHIAS CANAL-WEST

SERIKALI imetumia Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya kukarabati na kuongeza miundombinu ya elimu ya Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Butimba ni kati ya vyuo vilivyonufaika na jitihada za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu huku uongozi wa chuo hicho ukipongezwa kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali fedha.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mhe.Prof.Adolf Mkenda ameyasema hayo Oktoba 7, 2022 wakati akizungumza na menejimenti na watumishi wa Chuo cha Ualimu Butimba wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkenda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya elimu kwani muelekeo wa serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu umezidi kuimarika mara dufu.

“Tusiposema watu wanasahau, mazuri yanafanyika halafu tunasahau na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kupeleka fedha nyingi zaidi kwenye miradi ya maendeleo katika halmashauri,"amesema Waziri Mkenda.
Amewataka walimu na watumishi wote wa chuo hicho kuhakikisha kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali kwenye sekta ya elimu na shughuli zote za maendeleo huku akisisitiza kuwa changamoto katika sekta ya elimu haziwezi kukosekana lakini serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi.

Waziri Mkenda ameutaka uongozi wa Chuo cha Ualimu Butimba kuhakikisha kuwa unaendelea kusimamia miradi kwa uaminifu mkubwa huku akiupongeza kwa matumizi mazuri ya fedha zote za miradi.
Kadhalika Waziri Mkenda amempongeza Mbunge wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza, Mhe.Stanslaus Mabula kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jimbo lake hususani miradi ya elimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news