Mpira wa miguu ni burudani ndani ya burudani

NA DR.MOHAMED MAGUO

MPIRA ni sanaa na burudani ambayo ndani yake mna sanaa na burudani nyingi pia. Nikichukulia ushabiki tu ni burudani tosha.

Hasa katika ulimwengu huu wa kidijitali na mitandao ya kijamii ambapo tambo za mashabiki ni burudiani kweli kweli.

Nasema katika ulimwengu wa kidijitali kwa sababu zamani haikuwa rahisi kuona namna washabiki wa timu kama Simba na Yanga wanavyojibizana kama ilivyo hivi sasa.

Kupitia mitandao ya kijamii kama What's App, Facebook, Instagram, Telegram, Snap chart na mingine tunaziona tambo hizo vizuri sana kiasi cha kupata burudani ya semi, methali, nahau, simo, tenzi na vichekesho kupitia utani na furaha ya mashabiki.

Kimsingi, unaweza kuona namna ambavyo kabla ya mchezo kuanza tambo zinavyokuwa kwa wenye timu yaani mashabiki wa timu husika na kejeli zinavyokuwa kwa upande wa wapinzani wa timu husika.

Kwa hapa Tanzania tumeshuhudia Yanga akicheza na Al Hillal ya Sudan siku ya Oktoba 8,2022 na Simba ikicheza na De Agosto ya Angola siku ya Oktoba 9,2022.

Sanaa kabla ya mchezo na baada ya mchezo kupitia utani wa jadi ni burudani tosha. Kwa mfano, kabla ya mchezo baadhi ya washabiki ambao ni wa Yanga waliwananga washabiki wa Simba kwamba "leo mtatia aibu huko Angola."

Baada ya mchezo kwisha ikabadilika na ikawa "hakika leo mmecheza na kilaza." Katika kauli kama hizi za washabiki, ndani yake mnakuwa na lugha za aina kwa aina ambazo ni burudani tosha kwa masikio yanye kusikia.

Hakika, upo uwezekano mkubwa ikawa kuna watu si wapenzi wa kutazama mpira ukichezwa lakini wao burudani yao ni tambo na kejeli ambazo hutoka kwa watani wajadi.

Hii ndiyo inayonifanya niseme kwamba mpira una sanaa na burudani nyingi ndani yake. Acha ile burudani ya mchezo wenyewe uwanjani ambapo mtu atapigwa chenga, kanzu, tobo na pasi kama zile za Bacelona ya akina Inniesta na Messi lakini burudani ya tambo na kejeli, jazanda, picha, ishara, taswira, sitiari, tashibiha, tanakali sauti, nyimbo burudani nyingine ambayo utaipata mpirani.

Hakika, si katika makala haya mafupi naweza kutaja tambo na kejeli hizo kwa mifano na namna zinavyoburudisha lakini naahidi siku moja nitatoa makala dadavuzi kwenye eneo hili.

Simba na Yanga ni timu kubwa zenye kupendwa na Watanzania wengi na kupitia timu hizi tunapata burudani aina kwa aina. Tunazipongeza Simba na Yanga kwa hatua ziliyofikia tukiamini kwamba katika michezo ya marudiano zote mbili zitafuzu na kuendelea mbele.

WENU
Dkt. Mohamed Maguo
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Post a Comment

0 Comments