Mwajuma Nyamka amng'oa Bundala Wilaya ya Kibaha Mjini

NA ROTARY HAULE

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini mkoani Pwani, Maulid Bundala amejikuta akibwagwa vibaya katika uchaguzi wa kutetea nafasi yake uliofanyika Oktoba 2,2022 katika viwanja vya Filbertbay vilivyopo Mjini Kibaha.
Bundala ambaye amekaa madarakani katika vipindi vitatu sawa na miaka 15 kwa sasa alikuwa anagombea tena kipindi cha nne, lakini hata hivyo ameshindwa kufurukuta katika uchaguzi huo na hatimaye kujikuta akiangukia pua.

Katika uchaguzi huo nafasi ya mwenyekiti ilionekana kuwa ya moto kutokana na wajumbe kuingia ukumbini huku wakiimba wimbo mmoja wa kutaka kufanya mabadiliko ya kumtoa mwenyekiti huyo aliyepewa jina la Mzizi.

Bundala ,ameng'olewa katika nafasi hiyo kwa kujikuta akiambulia kura 172 dhidi Mwanamke Mwajuma Nyamka aliyeibuka kidedea kwa kupata kura 346 ,huku Sauda Mpambalioto akipata kura 33 na Abdallah Mdimu akipata kura 32.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kisarawe, Josephine Mwanga amesema, Mwajuma Nyamka ndiye mwenyekiti halali wa CCM Kibaha Mjini.

Mwanga amesema kuwa, katika uchaguzi huo kulikuwa na wajumbe halali 596 ambapo kura tano ziliharibika huku kura halali ni 583 lakini mshindi wa nafasi hiyo ni Mwajuma Nyamka aliyejizolea kura 346 na Maulid Bundala kura 172.
"Kwa mamlaka niliyopewa katika uchaguzi huu wa CCM Kibaha Mjini namtangaza Mwajuma Nyamka kuwa mwenyekiti kwa kupata kura 346 kwa kuwa ndiye mgombea pekee aliyepata kura nyingi kuliko wagombea wote,"amesema Mwanga.

Aidha,kundi la Vijana Halmashauri Kuu ya Wilaya walioshinda ni Nancy Matta ,Godlove Rwekaza,Valentine Mbawala na Mjata, wakati Mkutano Mkuu CCM Taifa ni Abasi Mtende(277), Method Mselewa(320) na Catherine Katele (436).

Nafasi ya kundi la Wazazi aliyeshinda ni Nobert Masebe(278) na Charles Maguye(292) huku kundi la Umoja wa Wanawake(UWT ) washindi ni Zuhura Sekelela (302),Maryam Sheiban (275),Hamo Machapula (271) na Elizabeth Ngoliga (266).
Bundala baada ya kushindwa uchaguzi huo,amesema anakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumpa nafasi ya kuongoza ndani ya miaka 15 lakini ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa mwenyekiti mpya aliyeshinda.

Nae Abdallah Mdimu amesema, anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanyakazi kubwa hapa nchini na kusema uchaguzi umekwisha lakini kikubwa na kwenda kufanykazi ya chama.

Mwingine ni Sauda Mpambalioto ambaye amesema kuwa kura zake hazikutosha lakini amempongeza Mwajuma Nyamka kwakuwa anastahili kutokana na kura nyingi alizopata ambapo ameahidi kutoa ushirikiano kwa ajili ya kujenga chama.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi mwenyekiti Mwajuma Nyamka,amesema kuwa anawashukuru wajumbe kwa kumpa heshima ya kumpigia kura nyingi za kuwa mshindi wa nafasi hiyo hivyo wategemee makubwa kutoka kwake.
Hatahivyo,Nyamka amesema anajua anadeni kubwa lakini atafanyakazi kwa bidii na juhudi kubwa kwa ajili ya kuleta umoja,upendo ,amani na ushirikiano katika chama kiwe imara zaidi katika uchaguzi wa mwaka 2024 pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news