MWANANGU ANA UWEZO WA KUIFANYA KAZI HIYO

NA ADELADIUS MAKWEHA

MWAKA 2012 Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani ilitayarisha Makala ya Magazeti ya Ujerumani iliyokuwa katika Makala ya Uchambuzi wa Tahariri za Magazeti hayo kwa kifupi, Makala haya iliuzungumzia uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati huo, Francois Bozize alipomteua mwanawe wa kumzaa Jeani Francoise Bozize(Junior) kuwa Waziri wa Ulinzi wa taifa hilo.

Makala hiyo iliyotayarishwa na gwiji la taaluma ya habari Abdul Mtulya na kusoma kwa pamoja naye na Bi.Frola Nzema, wote Mtulya na Nzema wakiwa ni watu wenye asili Tanzania, Mtulya akitokea Pwani naye Nzema akitokea Iringa, walipokuwa wakiyatayarisha makala haya mwanakwetu nilikuwa jirani nao katika chumba cha habari cha shirika hilo na hata walipokuwa wakiirekodi, ikiwa makala iliyosheheni viwango kadhaa vya ubora wa makala za redio na makala iliyopachikwa katika tovuti ya shirika hilo kongwe la utangazaji duniani.

Abdul Mtulya akiongoza kusimulia makala haya alinukuu maelezo ya Rais Francois Bozize yaliyonukuliwa kutoka katika tahariri za magazeti ya Ujerumani kuwa Rais Bozize amemteuwa mwanawe kuwa Waziri wa Ulinzi kwa sababu mwanawe huyu ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo.

“Mwanawe ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo, Naam hadi hapo ndipo na mimi naufunga ukurasa huu wa magazeti ya Ujerumani kwa leo, pamoja nami ni Frola Nzema na mimi Abdul Mtulya kutoka hapa Bonn.” Hivi ndivyo mtangazaji na mtayarishaji wa makala haya Abdu Mtulya alivyoufunga ukurasa huo wa makala haya ya siku hiyo.

Binafsi nilicheka sana nikajiuliza katika taifa lenye watu wanaokaribia milioni nne ni mwanae tu ndiye mwenye uwezo kuifanya kazi hiyo?

Mwanakwetu hiyo ndiyo ilikuwa dhana hata ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuiweka tahariri hiyo katika magazeti yao, nadhani ndiyo dhana ya mtayarishaji wa makala haya wakati huo kuiweka katika tahariri hiyo kwa msikilizaji wake.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa huyu mtoto wa Rais Bozize hakufanya vizuri kabisa katika uwaziri wake hadi aliondolewa na baba yake mwenyewe, huku Rais Bozize akinagwa na kusontwa kidole na wengi wakisema si ulisema mwanao ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo? Hali ilikuwa tete na Machi 24, 2013 Rais Bozize alipata misukosuko mikubwa kutoka kwa wanamgambo wa Seleka nayeye kutokomea nchini Cameroon.

Msomaji wangu kwa siku ya leo chukua dhana ya mtoto kuwa ni mtu uliye naye karibu, unayemfahamu, unayempenda na unayemuamini. Ichukue dhana hiyo kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati ya mwaka 2012 na kuileta katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2022, likiwa tukio la muongo mmoja uliopita.Upo mwanakwetu?

Nchini Tanzania, Oktoba 2, 2022 umefanyika uteuzi wa mawaziri wawili kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Waziri wa Tawala na Mikoa na Serikali za Mitaa.(TAMISEMI)

Miongoni mwao ni mheshimiwa Angela Kairuki, amechaguliwa kuwa mbunge na hapo hapo akachaguliwa kuwa Waziri wa TAMISEMI. Ndiyo kusema Mheshimiwa Kairuki amepewa vitu viwili kwa wakati mmoja. Waswahili wanasema wambili, havai moja;.Wambili ni wambili tu.

Ukilitazama Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la sasa lina wabunge wa CCM karibu 363/364, CHADEMA wabunge 20, ACT wabunge 4 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali 1.

Ukihesabu idadi ya wabunge walio mawaziri na manaibu inakaribia 48/49 Kwa tafsri ya kawaida anayefanya uteuzi huo hakuona mbunge wa kushika uwaziri wa TAMISEMI kutoka kwa kundi hilo la Wabunge hao zaidi ya 350 wasio mawaziri, manaibu naibu spika au spika na uteuzi huu umefanyika kutoka nje ya boma, hiyo ikiwa ni haki ya mteuaji.

Kwa ukweli wa Mungu ukitazama ndani ya boma hilo wapo wabunge wenye wenye sifa kedekede zaidi na maradufu ya Bi.Angela Kairuki kitaaluma, kiumri, kiuzoefu na hata kuifahamu serikali za Chama Cha Mapinduzi, lakini mteuaji ndiye mwenye maamuzi, mwanakwetu kama yale ya mwanangu ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo.

TAMISEMI ina changamoto nyingi sana kama vile hali mbaya ya mazingira ya shule mathalani uhaba wa vitendea kazi , changamoto ya zahanati zetu mazingira magumu ya watumishi wengi wa wizara hiyo, malalamiko yasiyofanyiwa kazi, kunyimwa kwa uhamisho kwa watumishi hao, watumsihi wa TAMISEMI kutolipwa stahiki kadhaa, watumishi wengi wanakaa vituo vya kazi muda mrefu bila ya kuhamishwa, viongozi wengi wa TAMISEMI kuwa mbali na watumishi wao, dhana mbaya kuwa Halmashauri kuna mchwa. Hayo na mengine mengi zikiwa ni changamoto zinazohitaji kutatuliwa kwa haraka na kinyume chake zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa TAMISEMI kama wale wanamgambo wa Seleka kule Afrika ya kati kwa Rais Bozize.

Mheshimiwa Angela Kairuki ana madeni makubwa sana ya kuwalipa Watanzania, kwanza kwa ubunge aliyopewa na pili kwa uwaziri wetu, asiende TAMISEMI kucheza sherehe, kinyume chake aliyemteua atasontwa kidole ilikuwaje awaache wabunge 350 akamteua mtu kutoka nje ya boma?

Mwanakwetu anaandika hivi siyo kwa dhana ya kumnanga mtu bali kukumbushana dhana ya kwenda kuwatumikia Watanzania kule walipo na nafasi hizi ni mali yao. Yasije kutokea yale ya kusema si ulisema mwanao ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo.

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news