MWANA NGEKEWA:Hii hapa simulizi ya kusisimua

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIKU moja nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari, niliamka mapema sana na kuendelea na ratiba zangu kama kawaida za shuleni za umma za bweni, lakini kwa kuwa haikuwa siku ya kuingia darasani, ulikuwa ni muda wa kufanya usafi na kujisomea wenyewe. 

Nilipokuwa najiandaa kwa shughuli hizo nilibaini kuwa hapo shuleni Same Sekondari kulikuwa mahafali ya Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (UKWATA) kidato cha nne.

UKWATA ukiwa ni Ushirika kwa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania, ulianzishwa kwa lengo la kuwasaidia na kuwalea vijana wa sekondari wanaosali makanisa ya Lutherani, Moravian na Anglican. 

Kwa kuwa haukuwa umoja wangu, mie sikuwamo katika maandalizi ya shughuli hiyo na ndiyo maana ratiba yangu ilikuwa ya usafi na kujisomea tu. 

Wakati wa kunywa uji wa asubuhi nilibaini kuwa vijana wa UKWATA walifanyia usafi na kudeki vizuri bwalo la chakula siku hiyo na sie uji tulinywea nje ya bwalo hilo la chakula na mikutano.

Kazi ya kudeki bwalo hilo ilikuwa ngumu sana kwa wanafunzi wote na mara nyingine wanafunzi watukutu walipewa adhabu hiyo, lakini wakati wa mahafali ya UKWATA - Ushirika kwa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania, TYCS -Tanzania Young Catholic Students, Umoja wa Vijana wa Kiislamu wa Sekondari na hata umoja wa Vijana wa Kisabato mara nyingi ufanyaji usafi wa bwalo hilo ulikuwa mwepesi na wa tija mno, hapo mwanakwetu nikibaini nguvu ya dini katika kufanikisha mambo makubwa. 

Hata kama umoja wa dhehebu ya dini ulikuwa na wanafunzi 10 kazi ya usafi wa bwalo ilifanyika vizuri mno na kwa wakati uliopangwa na sherehe kufanyika vizuri mno.

Mwanakwetu siku ya mahafali ya dini hata kama finyango ya nyama ikianguka sakafuni bwaloni unaweza kuiokota na kuila bila mashaka.

Siku za mahafali, kama wewe siyo siku ya mahafali ya umoja wako unaweza kubahatika kuingia katika mahafali hayo kwa sababu kadhaa; kwanza kwenda kushangaa kinachoendelea huko hapo unajialika mwenyewe, lakini pilau itakupiga chenga ya mwili, pili kama wewe ni kiongozi katika umoja wako basi mnaweza kualikwa viongozi wawili mwenyekiti na katibu wake na tatu wale viongozi wa serikali ya wanafunzi kaka mkuu anaingia moja kwa moja kuiwakilisha serikali yake. 

Kama yeye ni dhehebu lake anamtuma katibu wake kuiwakilisha serikali ya wanafunzi.

Siku hiyo mwanakwetu sikuwa na cheo chchote huko TYCS wala serikali ya wanafunzi, kwa ukweli halisi pilau ya UKWATA ilikuwa imenipiga chenga ya mwili. 

Vijana wa UKWATA walipamba bwalo hilo vizuri sana na jikoni harufu nzuri ya pilau ilinukia hadi mabweni kwetu huku kwaya zikiimba nyimbo mbalimbali, zingine kutoka katika redio kaseti na zingine za kuimbwa moja kwa moja.

Kengele ya chakula cha mchana ilipigwa na sie kujongea kuchukua ugali na maharage meupe, huku maharage haya meupe yalikuwa hayapendwi kabisa na wanafunzi wengi ikidaiwa kuwa magunia ya maharage hayo yalipigwa chapa ya maneno for pigs only, huku mwanafunzi aliyekuwa anatunza store ya chakula tuliyesoma naye darasa moja ndugu Elisante Elifasi akipingana na dhana hiyo. 

Ugali ulilika, lakini mawazo yote yalikuwa katika pilau la UKWATA, lakini tiketi za kuingia huko tayari zilishatupiga chenga, inakuwaje?.

Nyimbo za kwaya zilinivutia kutoka bwenini Mkwawa II na kushuka hadi bwaloni na kuingia kushangaa kile kinachoendelea, kwa bahati nzuri nilipofika bwaloni nilikuta foleni ya WANAUKWATA ikimalizika mithili ya mkiwa wa nyoka kichakani.

“Kwegas njoo uunge tela, pilau limejaa tele njoo njoo njoo haraka.” Kiongozi wa UKWATA alinialika na wezangu tulikuwamo bwaloni. Nilichukua pilau la UKWATA vizuri sana kuiweka katika chombo changu vizuri na kulifunika na kuendelea kufuatilia mahafali haya, kumbuka tumbo langu lilijaa ugali na maharage meupe. 

Kichwani mwangu nikijilaumu kula ugali huo na maharage, lakini pilau hilo nimelipata kwa bahati nasibu tu, mwanakwetu na mie mwana wa ngekewa.

Wakati mahafali haya yakiendelea yule kijana aliyekuwa na redio kaseti aliucheza wimbo mmoja wenye maneno haya, “Goliati alijifanya tishio, Goliati alijifanya tishio, Dhidi ya taifa la wana Israeli, Dhidi ya taifa la wana Israel…” Ulipochezwa wimbo huo ulinivutia sana, wakati sasa mahafali hayo yanakamilika huku wana UKWATA wakipiga picha na wachungaji wao nje ya bwalo.
Nilimsogelea kijana huyu ambaye alikuwa akisoma kidato cha tano nilimuomba kasha la kaseti ya albamu yenye nyimbo 13 iliyopewa jina Mwenye Mamlaka- Mapigano Ulyankulu Kwaya, kukiwa na nyimbo Goliati Alijifanya, Kuzaliwa Kwake, Mshindaye Mwenye Mamlaka, Neno la Mungu, Palikuwa na Mtu, Safari Yao, Siku ya Kutaabika, Tazama Mkono, Usimuhukumu Ndugu, Wakati Huo, Yatendeni, Yesu Akawambia na Zamani Ninyi.

“Hii ni kwaya ya ndugu kadhaa wakimbizi wenye asili ya nchi jirani, wapo huko Tabora wana nyimbo nyingi na nzuri.” Niliambiwa na kijana huyu aliyekuwa anacheza nyimbo hizo, kaseti yake ikiwa kando ikiwa imefunikwa na kitambaa chenye mauamaua huku sherehe ikifika ukingoni.

Mwanakwetu nilitoka hapo bwaloni huku nikuutafakari mno wimbo huo wa Goliati Alijifanya, pilau langu mkono katika kopo la kimbo, hatua kwa hatua hadi bwenini, mithili ya simba aliyepata windo mawindoni.

Baadaye nilibaini kuwa kwaya hii iliundwa na wakimbizi kutoka Burundi waliokua wakiishi Ulyankulu Tabora, mwanzoni mwa miaka ya 2000 serikali iliwahamisha na kuwapeleka kambi za wakimbizi zilizokuwepo Kigoma kama vile Nduta, Kanembwa na Nyarugusu wengine wakipata nafasi za kwenda Ughaibuni kama vile Marekani, Ulaya na Austria chini ya UNCHR ya Bi Sadako Ogata.

Huku baadhi yao wakibaki Tanzania, wakiishi hadi leo hii, wapo waliofariki dunia, yote hayo ni maisha ya binadamu. 

Kwa hakika ukipata nafasi ya uhai tenda wema, muombe Mungu, msifu Mungu, mwabudu Mungu na mshukuru Mungu na ukiondoka duniani watakaobaki watakukumbuka kwa wema wako.

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news