Serikali yawatoa hofu watumiaji wa kitimoto, yasema hiyo ni nyama salama

NA DOREEN ALOYCE

SERIKALI imewatoa hofu watumiaji wa nyama ya nguruwe maarufu kitimoto na kueleza kuwa nyama yake ni salama kama ilivyo nyama ya wanyama wengine.
Kitimoto kikiwa katika maandalizi.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania, Dkt.Stella Bitanyi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa shughuli za wakala katika mwaka wa fedha 2022/23.

Ametoa kauli hiyo kutokana na kuwepo na mkanganyiko wa maneno kuwa, mnyama huyo si salama kwa kuliwa kutokana na kile ambacho walikuwa wakieleza kuwa nguruwe ana wadudu wengi na hafai kuliwa.
Akitoa ufafanuzi, Dkt.Bitanyi amesema kuwa, nyama ya nguruwe ni salama kama ilivyo nyama ya wanyama wengine isipokuwa kinachotakiwa ni kuhakikisha mnyama huyo anapatiwa chanjo na dawa kama inavyotakiwa.

"Nyama ya nguruwe ni salama kabisa kama ilivyo nyama ya wanyama wengine kinachotakiwa ni kupatiwa tiba na chanjo zinazotakiwa,nguruwe anaminyoo ambayo ni mibaya endapo utaila inakuwa na tabia ya kuingia kwenye ubongo ambao unaweza kuvuruga ubongo,"ameeleza Dkt.Bitanyi.

Aidha, amesema kuwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Serikali ya Tanzania kupitia programu inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya inayoitwa Agri Connect imezindua kampeni ya kitaifa ya lishe bora ambayo ni mtaji ili kujenga tabia zinazofaa za milo nchini Tanzania kwa kutumia vyakula vinavyopatikana nchini.

Pia amesema katika kampeni hiyo suala zima la sumukuvu linalengwa kwa sababu katika vyakula vinavyopatikana hapa nchini ni jambo moja wapo linalochangia katika masuala ya usalama wa chakula.

"Chakula salama ni muhimu kwa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu,chakula kikiwa si salama, huathiri vibaya usalama wetu wa chakula na lishe, afya, makuzi ya watoto, na uwezo wa watu wazima kuongoza kwa tija maisha,"amesema Dkt.Bitanyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news