Wizara yaandaa mjadala wa Kitaifa kuhusu nishati safi

NA MWANDISHI WETU
 
WIZARA ya Nishati inatarajia kuandaa mjadala wa Kitaifa wenye lengo la kuleta suluhu ya namna Watanzania wanavyopika na kutafuta namna ya kupunguza au kuondoa kabisa matumizi ya nishati ya isiyo safi na salama.

Mjadala huo unatarajia kufanyika Novemba 1-2, 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini, Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nishati Januari Makamba alisema, mkutano huo utawakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za Afya, Nishati, Mazingira, Jinsia, Usawa watunga sera pamoja na sheria mbalimbali.

“Tatizo la namna Watanzania tunavyopika ni kubwa mno kuliko tunavyolijua, kuliko ambavyo tunalijadili; linaharibu mazingira, linadhoofisha afya linahusisha masuala ya jinsia pamoja na masuala ya usawa katika jamii,” alisema Makamba.

Alisema, Sera ya Nishati ya 2015 inayosimamiwa na Wizara ya Nishati inaelekeza Wizara ya Nishati kuchukua hatua za kuwawezesha watanzania kupata nishati safi na salama na kwa gharama wanayoimudu ili kuboresha ustawi wa watanzania kwa kiasi kikubwa.

Waziri Makamba alisema, Mjadala huo utaratibiwa na Wizara ya Nishati ili kupata majibu ya kudumu ya kuondokana na matumizi ya nishati ya kupikia ya mkaa na kuni nchini, pamoja na kupata uelewa wa pamoja juu ya suala nishati ya kupika hapa nchini.

Alisema, mjadala huo utasaidia kujua changamoto za kutumia kuni na mkaa, athari zilizopo na kuangalia matokeo yake.

Makamba alisema, Mifumo ya Kisera Sheria, Kikodi, Kifedha na Utawala itawekwa kwa ajili ya kupambana na hali ya namna tunavyopika na kuwaondoa watanzania kutumia nishati inaathiri Afya na Maisha.

Akizungumzia kuhusiana na madhara yanayojitokeza katika jamii juu ya matumizi ya kuni, mkaa na nishati nyingine zisizo safi na salama, Waziri Makamba alisema vituo vya afya nchini vimeelemewa na mzigo mkubwa wa utoaji huduma za afya za mfumo wa upumuaji zinazotokana na namna tunavyopika.

Alisema, Watanzania zaidi ya 33,000 wanafariki dunia kwa mwaka kutokana na kuvuta moshi wa namna tunavyopika chakula, hivyo hii inaendelea kuathiri akina mama na watoto wa kike kwa kupoteza muda mwingi kwenye kutafuta nishati ya kupikia ya kuni na Mkaa.

“Wanapokuwa wanatafuta nishati hiyo wanapunguza muda wa kutafuta elimu au kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali huko porini wanakutana na dhahama na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.”

“Pia, Nishati isiyo safi na salama inaleta utofauti au kutokuwa na usawa kati ya wanawake na wanaume, watu wa mjini na vijijini wenye kipato na wasio na kipato,” alisema Waziri Makamba.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Pauline Chale alisema, matumizi ya Nishati isiyo safi na salama inasababisha changamoto nyingi hasa katika Afya na matibabu yake ni gharama kubwa.

Dkt. Pauline alisema, magonjwa wa Mfumo wa upumuaji yanasababisha vifo vya watu wengi, na matumizi ya kuni, Mkaa na kinyesi cha wanyama vina sumu zaidi ya 200, “ndio maana watu wengi wanakuwa na macho mekundu kutokana na sumu hizi zinazopatikana kwenye moshi.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news