WCF yawamegea siri wajumbe kutoka Zanzibar

NA DIRAMAKINI

UJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ukiongozwa na mwenyekiti wake, Mhe. Mihayo Juma Nunga umetembelea ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) jijini Dar es Salaam kwa nia ya kubainisha masuala muhimu ya fidia.

Akizungumza baada ya kukutana na Watendaji wa WCF wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt.John Mduma, Mwenyekiti huyo amesema ziara hiyo imewawezesha kupata uelewa mpana wa namna Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi inavyotekelezwa na faida ambayo Watanzania wamepata kutokana na uwepo wa chombo hicho.

“Kwetu jambo hili ni geni bado halijatengenezewa utaratibu bora zaidi wa kuwalipa fidia wafanyakazi waliopata changamoto kwenye maeneo ya kazi, Zanzibar tuko katika maandalizi ya kutengeneza utaratibu wa jinsi gani mfanyakazi atapata fidia pindi anapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, kwa hivyo tukaona tutembelee Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao wana uzoefu mkubwa katika masuala haya nasi tuweze kuishauri serikali ili tuwe na chombo walau chenye uwiano na WCF,"amesema Nunga.

Amesema, wameona jinsi watu wengi walivyonufaika na uwepo wa WCF kwa hivyo ni wakati mwafaka kwa Zanzibar kuwa na Mfuko utakaotoa huduma bora kama ambavyo wameshuhudia hapo WCF.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw.Ali Nassor Shaaban amesema, mfuko huo uko katika maandalizi ya kuanzisha huduma kama hiyo ya kufidia wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

“Tumeona kabla ya kuanzisha chombo hicho ni vema kujifunza kwa wenzetu WCF ambao kwa kweli wamefanikiwa sana ili kujua sheria na kanuni zake zilivyo hatimaye tuwe katika nafasi nzuri ya kuanzisha chombo chetu kitakachotoa huduma kulingana na mazingira ya Zanzibar,"amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma ameema, WCF ina uzoefu wa miaka saba katika masuala ya utoaji fidia kwa wafanyakazi na imekuwa ni wakati mzuri wa kubadilishana mawazo ya namna bora ya kuendesha vyombo hivi vya Fidia kwa Wafanyakazi.

“Tumewaeleza namna tunavyotenda kazi katika miaka hii saba na mafanikio tuliyopata, tumejifunza mambo mengi ambayo wamekuwa wakituuliza na tunaamini wamejifunza mengi,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news