Rais Dkt.Mwinyi:Tuwekeze kitaalamu kufanikisha maendeleo nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekaribisha mashirikiano kati ya Serikali,wawekezaji na Taasisi za Kitaalamu katika Usimamizi wa Miradi, ili kufanikisha mipango ya maendeleo kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi.
Dokta Mwinyi ameelekeza hayo Oktoba 20, 2022, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka, wa Taasisi ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Miradi (PMI) Tawi la Tanzania, huko Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.

Amesema kuwa, Serikali zote mbili, ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinakaribisha mashirikiano mema na Taasisi hiyo, hali itakayowezesha kujenga ufanisi zaidi, katika usimamizi bora wa miradi, ili kufanikisha maendeleo ya nchi.
“Serikali zetu zote Mbili zimeridhishwa na juhudi za PMI Tawi la Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 katika kukuza uelewa wa kuwezesha uendeshaji bora wa Miradi, sambamba na utayari wa kujitolea kwao kushirikiana na Taasisi za Serikali pamoja na Sekta Binafsi, ili kuhakikisha tunafikia vigezo kupitia tafiti mbali mbali na kuwezesha mafanikio katika usimamizi wa miradi yenye tija,” amesema Dokta Mwinyi.

Amebainisha kuwa, kutokana na kuridhishwa huko, Serikali hapa Visiwani inakaribisha kwa mikono miwili hatua ya Utiaji Saini Makubaliano baina ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, pamoja na PMI Tawi la Tanzania, hatua ambayo inatarajiwa kutekelezwa hivi karibuni, ili kufanikisha Ujenzi wa Kituo maalum cha Ubora (Centre of Excellence).
Ameeleza kuwa, kituo kitakachokuwa chini ya wizara hiyo, kitasaidia utoaji wa mbinu, zana na nyenzo muhimu, zikiwemo za utoaji wa taaluma, stadi na mafunzo, yatakayopelekea usimamizi bora wa miradi yenye tija, na kwa ufanisi zaidi.

Ametaja kuwa ujuzi na utaalamu huo, ambao tayari Serikali na PMI wamewezesha hatua za awali za utekelezaji wake, unalenga kuwafikia wadau mbali mbali wakiwemo kutoka Sekta Binafsi, Watunga Sera pamoja na Jamii, ili kuchangia utoaji wa huduma bora katika usimamizi na uendeshaji wa miradi, ndani ya Nchi na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Rais Dokta Mwinyi amebainisha fursa nyingi ambazo zinapatikana Zanzibar, na ambapo Wataalamu na Wawekezaji kupitia PMI wanaweza kuzichangamkia, zikiwemo za Uchumi wa Buluu, Uvuvi, Mazingira, Kilimo, Uzalishaji, Vivutio katika Sekta ya Utalii, Biashara, Teknolojia ya Mawasiliano, Utamaduni, Huduma za Jamii, na Usafiri wa Baharini.
Hivyo amesema Mpango wa Maendeleo wa 2025 na ule wa Dira ya Zanzibar ya Mwaka 2050, sambamba na Dira ya Maendeleo Ya Tanzania 2025, na ile ya 2050, kwa pamoja na kwa kiasi kikubwa, inategemea kiwango cha ubora, ustadi, maarifa, utaalamu na uwajibikaji, mambo ambayo yakikosekana, Taifa litashuhudia Miradi mingi ya Maendeleo ikishindwa kuleta tija, kinyume na matarajio, kutokana na kufeli usimamizi wake.

“Hivyo pia, ni pamoja na ukweli kwamba, kutokana na maendeleo ya teknolojia, utandawazi, na uwepo wa miradi mikubwa ya kimaendeleo ulimwenguni, hatuna budi kuwa na wataalamu wa kutosha na weledi katika uendeshaji bora wa miradi, Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, na hilo ni jambo la umuhimu wa pekee,”ameongeza Dokta Mwinyi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mheshimiwa Mudrik Ramadhan Soraga, ameshukuru hatua ya PMI kuuleta Mkutano huo muhimu hapa Zanzibar, ambapo faraja yake ni pamoja na kuhamasisha utekelezaji na uwekezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo, ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Ameeleza kuwa, nafasi ya kuwekeza hapa Visiwani kwa sasa inahamasishwa na mazingira bora ya amani, utulivu na maridhiano ya kisiasa na kwamba wawekezaji waje kuungana na Serikali katika kusaidia utoaji wa fursa muhimu kwa wananchi, ili kujiletea maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa PMI Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. George Asamani, ameeleza kuwa lengo la Taasisi yake, pamoja na kufanyika kwa Mkutano huo hapa Visiwani, ni katika juhudi za kuisogeza Afrika katika hatua za juu za maendeleo, kupitia usimamizi na uteuzi bora wa miradi yenye tija.

Hata hivyo ameeleza kwamba, kama ilivyokuwa kwingineko ulimwenguni, Taasisi yake haikunusurika kutokana na wimbi la kuyumba kwa Uchumi wa Dunia, kulikosababishwa na mambo mbali mbali yakiwemo Janga la UVIKO-19.

Katika salamu zake za ukaribisho, Rais wa PMI Tanzania, Bi.Ella Naiman, ameeleza kuwa Taasisi hiyo ni kiunganishi kati ya Uwekezaji, Uchumi wenyewe, na Jamii kwa upana wake, na hivyo umekuja wakati muafaka ambapo Zanzibar ikipania katika utekelezaji wa dira yake ya kuwekeza katika Uchumi wa Buluu.
Ufunguzi wa Mkutano huo wa Siku Mbili, uliowajumuisha Mawaziri, Viongozi wa Serikali, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Mashirika ya Kimataifa, Makampuni, Wawekezaji na Washirika wa Maendeleo, pamoja na Washiriki wa Taasisi za Kusimamia Miradi, kutoka ndani na Nje ya Nchi, umehusisha pia harakati mbali mbali, zikiwemo za Vikundi vya Burdani, zikiongozwa na Ngoma ya Msewe ya Kikundi cha Taifa cha Sanaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news