NA FRESHA KINASA
WAVUVI katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamejitokeza kwa wingi kujisajili ili waweze kupatiwa mikopo na Serikali kwa lengo la kuanzisha mashamba ya ufugaji wa samaki na ununuzi wa zana bora za uvuvi zitakazowapa ufanisi na tija katika utekelezaji wa shughuli zao za uvuvi wa samaki ndani ya Ziwa Victoria.
Wameyasema hayo wakati wakizungumza na DIRAMAKINI wakiwa katika zoezi la kujisajili ambapo pamoja na mambo mengine wametoa pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Samia Hassan kwa hatua hiyo njema.
Wamesema, hatua hiyo itawawezesha kufanya shughuli za uvuvi kwa tija na hivyo kujiletea maendeleo yao na kuchochea ukuaji wa maendeleo ya taifa.
Jane Joseph mkazi wa Kata ya Kiriba Wilaya ya Musoma amesema Rais Samia ameonesha upendo wa dhati kwa wavuvi na kutaka kuwakwamua kiuchumi kupitia uvuvi wa kisasa utakaotumia zana bora.
Ambapo amesema, mikopo hiyo italeta mageuzi chanya kwa wavuvi wakiwemo wanawake wanaofanya kazi hiyo jambo ambalo amesema awali halikufanyika isipokuwa katika uongozi wake wa awamu ya sita.
Kwa upande wake Mathias Peter amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inapaswa kupongezwa kwani imetambua umuhimu wa Sekta ya Uvuvi na hivyo kuamua kutoa fedha za kuwakopesha kwani kilio cha wavuvi wengi ilikuwa ni matumizi ya zana duni ambazo kwa muda mrefu wamekuwa wakizitumia.
"Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira njema ya kutujali wavuvi tunaipongeza sana. Ni mara ya kwanza sekta ya uvuvi kuwekewa fedha na wavuvi kuaminiwa kuweza kukopesheka kilio kikubwa cha wavuvi ni kutumia zana zilizopitwa na wakati pongezi kwa Rais Samia Hassan na Mbunge wa Jimbo letu la Musoma Vijijini Prof.Muhongo kwa maono bora ya kutusaidia tuweze kupiga hatua katika kazi zetu Mungu awabariki sana tunaamini tutafanya uvuvi wa kisasa na wenye manufaa makubwa,"amesema Peter.
Imani Kapinga ni Mkurugenzi wa Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji ambapo amesema Halamashauri ya Wilaya ya Musoma ni miongoni mwa halmashauri nyingi wanazozitembelea kwa zoezi la kuainisha wanufaika na kupitia maandiko ili wavuvi waweze kunufaika mradi huo ambao Mheshimiwa Rais amepata fedha kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuweza kuwakopesha wavuvi.
Amesema, pia fedha hizo zitasaidia wakuzaji viumbe maji pembejeo mbalimbali za kisasa kuongeza uzalishaji wa samaki Tanzania kwa ajili ya kuboresha lishe, kuongeza kipato na kunufaisha taifa.
Aidha, taarifa ya Jimbo la Musoma Vijijini iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimwa Prof. Sospeter Muhongo imetoa pongezi pia kwa Serikali kufuatia uamuzi wa kutoa mikopo isiyokuwa na riba.
"Samaki wamepungua sana, kwa hiyo uamuzi wa Serikali wa kutoa mikopo isiyokuwa na riba ni uamuzi mzuri sana.kwani mikopo hiyo itaenda kubadili mitindo ya uvuvi ndani ya ziwa hilo. Muhimu sana ni kuanzishwa kwa uvuvi wa vizimba (cage fish farming aquaculture) ambao ni wa kisasa na wenye uvunaji mkubwa wa samaki,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, kwa mujibu wa taarifa hiyo imefafanua takwimu muhimu za Ziwa Victoria ambapo umri ni miaka 400,000, ambapo ujazo wa maji ni takribani Cubic 2, 424 kilometers, na jumla ya aina ya samaki zaidi ya 500.