'Rais Samia amefungua nchi na kuimarisha diplomasia, kaleta fursa na kuimarisha uchumi na misingi bora ya uongozi'

NA DIRAMAKINI

VIONGOZI na wadau mbalimbali leo Oktoba 15, 2022 wameshiriki katika Mkutano wa Zoom ulioandaliwa na Watch Tanzania huku ukirushwa mubashara na vyombo mbalimbali vya habari.Mjadala huo ulikuwa sehemu ya kumbukizi ya miaka 23 bila Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule ilikuwa Tanganyika).

Oktoba 14, 1999, ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe kwani Mwalimu Nyerere aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St.Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua kansa ya damu.

Mwili wa Mwalimu Nyerere ulipokelewa jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani jijini humo.

Oktoba 20, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao.

Aidha,Oktoba 21, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria ibada hiyo. Watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi Oktoba 22, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya maziko.

Maziko ya Mwalimu Nyerere yalifanyika Oktoba 23, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika Kijiji cha Butiama, wilayani Musoma Vijijini, mkoani Mara.Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alikua akiamini katika falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Aidha, mkutano huu wa leo ulikuwa ukiongozwa na mada ya Utekelezaji wa Falsafa za Mwalimu Nyerere katika Serikali ya Awamu ya Sita. Awamu hii inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Wamesema kuwa;

BALOZI OMBENI Y. SEFUE, MWENYEKITI WA BODI YA UONGOZI INSTITUTE

"Binafsi ninamsifu sana Rais wetu Mhe.Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani ameweza kutembea na philosopia (falsafa) za marais wote na kuziunganisha pamoja, Nyerere (Hayati Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) aliweka misingi ya uongozi, Mwinyi (Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi) alifungua nchi, Mkapa (Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa) alidhibiti mianya ya unyang'ang'i, Kikwete (Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete) alifungua Taifa, Magufuli (Rais mstaafu wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli) alijenga miundombinu na Rais Samia amefungua nchi na kuimarisha diplomasia, kaleta fursa na kuimarisha uchumi na misingi bora ya uongozi;
"Kuonesha kwamba Hayati Mwalimu Nyerere aliweka misingi bora sana ni pale tulipotoka kwenye Awamu ya Tano kwenda na Sita ingekuwa nchi nyingine Afrika huko, kungekuwa na vurungu sana na kutokuelewana, ila sisi ni misingi ndio iliyotuongoza na tukakabidhiana madaraka bila wasiwasi na taifa sasa linazidi kusonga mbele
"Mwalimu Nyerere alisema uongozi bora sio tu kupambana na rushwa na mafisadi bali uongozi bora ni ule unaojali watu wake, kutaka kutatua shida zao na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba nchi, haya yote tuliyaona kwa Mwalimu Nyerere pia tunayaona kwa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan."

BALOZI DKT.ASHA-ROSE MIGIRO, BALOZI WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA

"Ushirikiano wa vyama ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ilisaidia sana kuimarisha diplomasia ya nchi, mfano chama cha TANU kilishirikiana na Chama cha ASP katika kujenga nchi pia kuna vyama kama KANU, UPC na vingine vya nje ya Tanzania vilishirikiana katika kujenga nchi na misingi ile iliyowekwa ndio inaifanya nchi hizi bado ziendelee kuwa na mahusiano mazuri.
"Moja ya sera ambayo ilikuwa ni moja ya misingi ya taifa letu ni sera ya kutokufungamana na upande wowote, nchi hii itakuwa na uhuru wa kuchagua kushirikiana na nchi ipi bila kuamuliwa.

" Hayati Mwalimu Nyerere aliliongoza taifa letu kupaza sauti yake kutetea wote waliokandamizwa na ukoloni, ubaguzi wa rangi na kutaka uhuru kuwa haki ya msingi ya taifa lolote".

DKT. AYOUB RIOBA, MKURUGENZI MKUU TBC

"Falsafa ya Ubuntu ni ile Falsafa inayojali utu na haki za watu na Falsafa hii iliweza kutumika sana kipindi cha Awamu ya Kwanza ya Hayati Mwalimu Nyerere, lakini pia Falsafa hii tunaiona kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwani amekuwa kiongozi wa kujali maisha ya watu na kuangalia namna ya kutatua changamoto zao.
"Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi sana kusimamia rasilimali kwa ajili ya Watanzania na kizazi kijacho, mfano mzuri ile Filamu ya Royal Tour imesaidia sana watalii kuijua Tanzania na kuja kwa wingi lakini pato lake litaisaidia katika kuhifadhi zaidia Rasilimali kwa kizazi kijacho.
"Tanzania ya sasa sio sawa na ile Tanzania ya mwaka 1960, Tanzania hii ya sasa ni taifa linalozidi kuendelea na kutanua mahusiano yake zaidi na nchi zingine, hii inaonesha Taifa letu lina viongozi imara na wanaojitambua na kujua tunatoka wapi na tunataka kwenda wapi."

ANTHONY MTAKA, MKUU WA MKOA WA NJOMBE

"Miaka 30 nyuma kuna magonjwa katika familia ukipata tulikuwa tunashikana uchawi, leo hii huwezi kuona hilo kwa sababu Mhe.Rais ameweza kununua mashine kubwa na mitambo ya kisasa kabisa katika hospitali zetu za kanda, mikoa na wilaya mtu akiumwa inatuambia ni ugonjwa gani.
" Vijana inabidi tubadilike sana, wengi wetu tunapewa dhamana ya uongozi halafu tunafanya tutakavyo, vijana wengi wakipata kazi hasa mijini na vijijini wanakwenda kuwa walevi wa madaraka na kutumia vyeo vyetu kwa maslahi yetu na sio Taifa.
"Mwalimu Nyerere aliamini katika miundombinu kusudi Taifa hasa mikoa iweze kushirikiana lazima miundombinu iwe safi, mahindi yanalimwa Rukwa ila yanatumika Dar es Salaam hii ni kwa sababu ya ubora wa miundombinu, tunamsifu Rais Samia kwa kujitahidi kuzidi kuendeleza miundombinu hasa ya barabara, majini, anga na reli."

GOODLUCK NG'ING'O, MCHAMBUZI WA MASUALA YA KISIASA, UCHUMI NA KIDIPLOMASIA

"Maridhiano, mabadiliko, ustamilivu na kujenga taifa ni baadhi ya misimamo na maamuzi ambayo Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiyazingatia nje na matarajio ya watu wengi ndani ya chama na nje ya chama.
"Rais wetu ameonesha kuwa ni mtu wa msikivu na mpenda maridhiano yapo mengi ambayo amewashangaza wengi mfano mzuri ni kuruhusu kuundwa kwa kamati itakayofanya mapitio ya katiba ambapo watu wengi sana hasa wanachama wa CCM walijua sio muda sahihi kulizungumzia ila Rais alikuwa msikivu na kulipa sikio la tatu ila kwa kufuata utaratibu mzuri."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news