Maagizo ya Rais Samia ya nchi kujitosheleza kwa sukari yanukia, Waziri Mkuu abainisha mengi

*Aupongeza uongozi wa Kagera Sugar kwa kuwa na historia nzuri ya ulipaji kodi

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya nchi kujitosheleza kwa uzalishaji wa sukari yameanza kunukia baada ya uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar kuongeza uzalishaji na kufikia tani 110,000 kutoka tani 60,000.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia magunia ya Sukari ndani ya ghala, wakati alipofanya ziara ya kukagua upanuzi wa mashamba ya miwa na mitambo na iliyoongezwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho, kilichopo Misenyi Mkoani Kagera. Oktoba 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa pongezi hizo leo Jumamosi, Oktoba 15, 2022 alipofanya ziara ya kukagua upanuzi wa mashamba ya miwa na mitambo na iliyoongezwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Kagera Sugar, Misenyi Mkoani Kagera.

Amesema kitendo cha kampuni hiyo kuendelea kuweka mikakati ya kuboresha na kukuza uwekezaji ni kizuri kwani kwa kiasi kikubwa kitawezesha kuongeza kiwango cha uzalishaji wa sukari nchini na kuipungua Serikali gharama ya kuagiza kutoka nje.

Waziri Mkuu amesema kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni fursa ya kiuchumi kwa wakazi waishio katika vijiji jirani na kiwanda hicho ambao wanajiajiri kupitia kilimo cha miwa kwa kuwa wana uhakika wa soko kiwandani hapo. “Endeleeni kuiunga mkono Serikali kwa kuongeza fursa za ajira kupitia kiwanda chenu.”

“Uwekezaji wenu utawezesha kuongeza kiwango cha uzalishaji wa sukari nchini, hii itawezesha nchi kupunguza kiwango cha sukari tunachoagiza kutoka nje. Mkakati wenu wa upanuzi wa kiwanda uende sambamba na ushirikishwaji wa wananchi waishio katika vijiji vinavyowazunguka ili nao waongeze mashamba ya miwa.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Wilson Sakulo ahakikisha anaweka mkakati wa kuhamasisha wananchi wa vijiji 13 vinavyozunguka kiwanda hicho kulima zao la miwa kwa wingi ili kuweza kujiongezea kipato na kuongeza idadi ya malighafi inayohitajika kiwandani hapo.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha yale yote yaliyo ahidiwa yanatekelezwa. “Viongozi wangu wa CCM sisi tutaendelea kumsaidia Rais Samia kuhakikisha yote yaliyoahidiwa yanatekelezwa.”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji hao kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ili malengo waliyoyaweka katika uwekezaji huo yaweze kufikiwa na kuongeza tija kwao na Taifa kwa ujumla.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kusimamia kikamilifu sharia za ukusanyaji wa mapato nchini.

“…Yeyote aliyeamua kufanya biashara nchini ahakikishe suala la kulipa kodi analipa kipaumbele. TRA chukueni hatua kwa mfanyabiashara atakayebainika kukwepa kodi.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza TRA kuwafuatilia wafanyabiashara wanaotumia vibaya majina ya viongozi wakiwemo wa kitaifa kukwepa kodi wanazotakiwa kuzitoa kwa Serikali kwa kuwa kila anayefanya biashara nchini hata kama ni kiongozi anapaswa kulipa kodi.

”TRA endeleeni kuchukua hatua hata kwa kumfuata kiongozi aliyetajwa ili mjiridhishe kama kinachosemwa na mfanyabiashara ni sahihi, kwasababu matumizi mabaya ya majina ya viongozi yanawasumbua sana watumishi wa TRA.”

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Kagera Sugar, Seif Ali Seif alisema kiwanda chao kimefanikiwa kuongeza uzalishaji ambapo wanatarajia kuzalisha tani 110,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tofauti na miaka mitano iliyopita ambapo walikuwa wanazalisha tani 60,000 kwa mwaka. Lengo letu ni kuzalisha tani 300,000. Kiwanda kwa sasa kimeajiri watumishi 10,000.

Pia, Mwenyekiti huyo aliishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja la Kitengule ambalo linaunganisha wilaya za Misenyi na Karagwe kwani licha ya kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa wilaya hizo pia litawawezesha kusafirisha malighafi za kiwanda kwa urahisi kwa kuwa baadhi ya mashamba yao yapo wilayani Karagwe. “Ujenzi wa daraja hili unatupa fursa ya kuendelea kuongeza mashamba ya miwa.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news