Rais Samia ataka sheria kutoa kipaumbele kwa wanawake

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inahitaji Sheria madhubuti kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na umiliki wa rasilimali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi pamoja na Wageni mbalimbali katika Maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) kwenye hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Oktoba, 2022. (Picha na Ikulu).

Rais Samia amesema hayo Oktoba 20,2022 kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Women in Law and Development in Africa – WiLDAF) yaliyofanyika ukumbi wa Serena.

Aidha, Rais Samia amesema licha ya takwimu kuonyesha kuwa asilimia kubwa ya wanawake wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji, bado baadhi ya mila na desturi zinawafanya wanawake kuendelea kukandamizwa.
Rais Samia pia amesema Sheria ni nyenzo kuu ya ufikiwaji wa usawa wa kijinsia na ustawi wa wanawake hivyo kutoa kipaumbele kwa wanawake ni jambo la lazima ili kuleta maendeleo.
Vile vile, Rais Samia amesema ipo haja ya kufanya tathmini ya Sheria zilizopo na kuona zina mchango gani kwa Watanzania na kuhakikisha kuwa zinakwenda ngazi za chini ili ziweze kutambuliwa na kufahamika kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa Sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kurahisisha kutoa elimu na ufahamu kwa wananchi.
Rais Samia ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Wasaidizi wa masuala ya Sheria kuwashirikisha wananchi na viongozi wa dini na kimila katika kuondoa vitendo vya udhalilishaji na ukandamizaji dhidi ya mwanamke.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news