Rais Samia,Ruto watoa maagizo kwa mawaziri

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kenya,Mheshimiwa Dkt.William Ruto wametoa maagizo kwa mawaziri wa uwekezaji kuhakikisha wanaondoa vikwazo mbalimbali vya biashara baina ya mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki.

“Kazi hii ilianza na Rais mstaafu, Uhuru Kenyata (Rais wa Jamhuri ya Kenya) na tulikubaliana kwa kuwataka wataalamu wetu kufanyia kazi vikwazo vya biashara vilivyopo, mawaziri hao walitambua vikwazo 68 na vilifanyiwa kazi 54 na tumewataka sasa mawaziri wetu wakutane na kufanyia kazi vikwazo hivyo ili kuwe na uhuru wa kibiashara.

“Tanzania na Kenya tusigawane umaskini na udhalili, lakini tugawane utajiri tutakaofanya kupitia biashara,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni kati ya mambo waliyojadiliana kutafutiwa ufumbuzi wa haraka kwa maslahi ya pande zote mbili. Ni katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt.Ruto tangua aingie madarakani hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Kenya,Dkt.Ruto amesema mabishano yaliyokuwepo kati ya Tanzania na Kenya wameyaweka kando, kwani, wanataka kujenga uchumi wa pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na yapo mengi watayafanya wakiwa pamoja kuanzia sasa.

“Ile historia ya zamani kidogo mabishano tumeyaweka nyuma yetu, tunataka kujenga mahusiano mema, tunataka Watanzania wafaidike na tunataka Wakenya wafaidike, Wakenya wakifaidika na sisi, Tanzania itafaidika.

“Rais atahesabu ushirikiano wangu, Serikali yangu ipo tayari kufanya kazi kwa maslahi ya nchi zetu mbili, tumekubaliana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kushirikiana kuangalia makosa yanayovuka mipaka, madawa ya kulevya (dawa za kulevya), uharamia, ujangili na usafirshaji wa watu,”amesema Mheshimiwa Rais.

Naye Rais Samia amesema Tanzania na Kenya zinapata taswira mbaya ya usafirishaji wa binadamu, kwani kinachofanyika ni kuwakamata wahalifu pekee lakini kwenye rekodi za Dunia taswira inakuwa mbaya, "kuna haja kuchukuliwa hatua kudhibiti zaidi bishara hiyo,"amesema Mheshimiwa Rais.

Rais Dkt.Ruto amesema, Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania akibainisha kwamba, kuondoshwa kwa changamoto hizo kumeinufaisha zaidi Tanzania ikilinganishwa na Kenya.

Mheshimiwa Rais amesema biashara baina ya Tanzania na Kenya imezidi kuimarika ambapo usafirishaji wa bidha kwa mwaka mmoja imepanda kutoka shilingi bilioni 27 kutoka Tanzania na kufikia shilingi bilioni 50 kwenda Kenya.

Amesema,kwa upande wa Kenya usafirishaji wa bidhaa kutoka Kenya kuja Tanzania imepanda kutoka shilingi bilioni 31 hadi kufikia shilingi bilioni 45.

“Leo tunanunua vitu vingi kutoka Tanzania kuliko wanavyonunua kutoka Kenya na hii ni kutokana na ushirikiano baina ya nchi zetu,"amesema Rais Dkt.Ruto.

Rais Ruto amesema Mawaziri baina ya Kenya na Tanzania wanapaswa kufanyia kazi changamoto zilizobaki na kufikia mwishoni mwa mwaka huu changamoto zote zimetatuliwa.

Mbali na hayo amesema,Serikali yake inakusudia kuendelea na ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, hadi Pwani ya Mombasa na baadaye jijini Nairobi.

Rais Dkt.Ruto amesema,mpango huo utatekelezwa ili kupunguza gharama za nishati ambapo mradi huo utashusha gharama za umeme kwa viwanda na matumizi ya nyumbani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news