Ridhiwani Kikwete atembelea banda la BRELA huku akitoa rai kwa vijana

NA ROTARY HAULE

NAIBU Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ametembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) huku akisifu wakala huo kuwa kazi wanayofanya inaleta mchango mkubwa wa maendeleo kwa Taifa.
Kikwete ametoa kauli hiyo Oktoba 9,mwaka huu katika maonesho ya tatu ya uwekezaji na biashara yanayofanyika katika eneo la stendi ya zamani ya Mailimoja Kibaha mkoani Pwani.

Maadhimisho hayo ambayo yamesimamiwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TAN TRADE) yamekuwa na mwitikio mkubwa kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Akiwa katika banda la BRELA, Mheshimiwa Kikwete,amesema BRELA wana mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo hasa katika kupitia biashara na uwekezaji na kwamba juhudi wanazofanya lazima ziendelee kwa faida ya Taifa.

"Kwa kweli BRELA wanafanya kazi kubwa sana ya kusajili majina makampuni,leseni na biashara na kupitia wao tumeona mhamko mkubwa wa ongezeko la mapato ya Taifa kupitia kampuni zilizosajiliwa hivyo lazima Serikali iendelee kuunga mkono taasisi hiyo,"amesema Kikwete.

Aidha, Kikwete ametumia nafasi hiyo kugawa vyeti kwa wananchi waliosajili kampuni zao BRELA katika kipindi cha maonesho hayo huku akiomba wananchi kutumia fursa hiyo kikamilifu.

Mbali na hilo lakini pia Kikwete,amewaomba vijana kufika katika banda la BRELA kwa ajili ya kusajili kampuni zao kwa kuwa wakifanya hivyo watakuwa wamejihakikishia usalama wa kampuni zao na kazi wanazofanya.
Amesema kuwa,wapo vijana wamekuwana ndoto za kumiliki kampuni kubwa lakini wanashindwa namna ya kufikia malengo hayo na badala yake hutumia majina yao bila kusajili jambo ambalo wakati mwingine linawanyima haki zao.

"Mimi nawashauri vijana kuitumia taasisi ya Brela ili kusajili kampuni zao kwakuwa wakifanya hivyo watakuwa wamesimama imara na kazi zao wanazofanya zitakuwa zimelindwa na hakuna usumbufu watakaopata,"ameongeza Kikwete.

Kwa upande wake Afisa Sheria wa BRELA, Aneth Mfinanga amesema kuwa, kwa sasa BRELA imekuja na teknolojia mpya na mtu akifika katika banda lao anaweza kusajili na kupata cheti chake papo hapo bila usumbufu.

"Kwa kweli toka tumefika hapa Oktoba 5 BRELA imepata mafanikio makubwa kwa kuwa idadi ya makampuni,leseni na majina ya biashara tuliyosajili mengi na mhamko umekuwa mkubwa zaidi," amesema Mfinanga.
Amesema,BRELA wataendelea kutoa huduma hiyo katika mikoa yote hapa nchini huku akisema mkoa wenye kufanya maonesho ya aina yoyote ni vyema wakashirikisha taasisi hiyo ili kuweza kusogeza huduma kwa jamii.

Hata hivyo, Mfinanga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya Mkoa wa Pwani kwa namna walivyojipanga katika kuwasaidia wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi hii.

Post a Comment

0 Comments