SERENGETI GIRLS: KOFIA TWAWAVULIA

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Oktoba 18, 2022 timu ya Soka ya Taifa ya Wasichana chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Girls) imefuzu kuingia robo fainali Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri huo, michuano inayoendelea huko nchini India.

Mafanikio haya yanakuja licha ya awali, Serengeti Girls kuanza vibaya michuano hiyo kwa kuchapwa 4-0 na mabingwa watetezi, Japan ingawa mechi iliyofuata katika Kundi lao la D Uwanja wa Jawaharlal Nehru, Margao, Goa nchini India walilipiza kisasi kwa Ufaransa.

Ni kwa kuikung'uta mabao 2-1, hivyo kujizolea alama zote tatu huku leo ndani ya Uwanja wa DY Patil Mumbai ikionesha tena juhudi na maarifa kwa kwenda sambamba na Canada kwa bao moja kwa moja, hivyo kuwaondosha Canada katika michuano hiyo.

Kwa matokeo haya, Tanzania sasa inaungana na Japan katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa Kundi D, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, huu ni ushindi wa Taifa na heshima kubwa kwa Taifa, hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kuendelea kuwaombea Serengeti Girls waweze kusonga mbele, endelea hapa chini;


1:Hawa ni watoto wetu, na sisi wazazi wao,
Ni wawakilishi wetu, inabamba kazi yao,
Waleta furaha kwetu, kwa mafanikio yao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

2:Kwamba Robo fainali, wameshaingia wao,
Kwa kucheza mechi kali, kombe la dunia lao,
Ni furaha kweli kweli, kwetu Zaidi ya kwao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

3:Tunasema Tanzania, wala sasa sio wao,
Robo tumeshaingia, sababu ya kazi yao,
Sana tunafurahia, kwa kutoa jasho kwao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

4:Kwenye zao mechi tatu, uwanjani peke yao,
Matokeo ni matatu, Robo Fainali hao,
Pokeeni shangwe zetu, njema kuzidi mafao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

5:Japan na Tanzania, haikuwa mechi yao,
Kadi nyekundu sikia, liharibu mechi yao,
Tulijisikitikia, kwa kushindwa mechi yao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

6:Ufaransa-Tanzania, siku yetu mechi yao,
Jinsi walivyopania, liona juhudi zao,
Juhudi zilizidia, kupata ushindi wao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

7:Canada na Tanzania, ama zetu ama zao,
Wasichana kuingia, meona mchezo wao,
Pale wameshikilia, sasa sifa nyingi kwao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

8:Inapaa Tanzania, sababu ya kazi yao,
Wakifanyacho India, zitadumu sifa zao,
Kumbukumbu Tanzania, taimba majina yao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

9:Hongera kwa wachezaji, benchi la ufundi lao,
Mama Samia mtaji, kwa hamasa zake kwao,
Nasi washangiliaji, tusuke mataji yao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

10:Robo Fainali sasa, heri zote zende kwao,
Wakacheze kwa hamasa, matokeo yawe yao,
Nusu fainali hasa, nayo ibakie kwao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

11:Ndani ya mwezi mmoja, sio wao peke yao,
Robo fainali moja, Tembo Warriors nao,
Hongera hizi pamoja, zote wazipate wao,
Ni Serengeti Girls, kofia twawavulia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news