Serengeti Girls wamkosha Rais Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekipongeza kikosi cha timu ya Serengeti Girls kwa kufuzu robo fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia kwa Wawanawake chini ya Miaka 17.

Ni kupitia michuano inayoendelea huko nchini India ambapo leo Oktoba 18, 2022 vijana hao wa Serengeti Girls kupitia Kundi D ndani ya dimba la DY Patil jijini Mumbai wametoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Canada.

Bao la Serengeti Girls lilifungwa dakika ya 35 na Veronica Gabriel Mapunda huku lile la Canada likifungwa na Amanda Marie Allen dakika ya 14.

"Mmenifurahisha sana watoto wangu Serengeti Girls kwa kuandika historia ya kufuzu kuingia robo fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya miaka 17 nchini India. Mmefanya jambo kubwa kwa nchi yetu Tanzania na nawatakia kheri katika hatua ya robo fainali,"ameeleza Mheshimiwa Rais Samia.

Awali pia Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe.Mohamed Mchengerwa naye ameipongeza Serengeti Girls kwa kufuzu kuingia robo.

"Kwa niaba ya Serikali ninapenda kupongeza Sana timu yetu ya Serengeti Girls kwani wametambua kuwa wana wajibu mkubwa wa kuiwakisha Tanzania katika mashindano haya.

"Hapa ni lazima nimshukuru Mhe.Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwa maelekezo ya mahususi na kipaumbele anachotoa kwenye sekta hii,"amebainisha Waziri Mchengerwa.

Hii ni historia ya kipekee kwa Serengeti Girls ambao awali walianza vibaya michuano hiyo kwa kuchapwa 4-0 na mabingwa watetezi, Japan.

Aidha,mechi iliyofuata katika Kundi lao la D Uwanja wa Jawaharlal Nehru, Margao, Goa nchini India walilipiza kisasi kwa Ufaransa kwa kuichapa mabao 2-1

Kwa matokeo haya, Tanzania sasa inaungana na Japan katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa Kundi D huku Watanzania wakiiombea iweze kusonga mbele zaidi kwani licha ya mafanikio hayo pia wanalitangaza Taifa katika anga za Kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news