Serikali yadhamiria makubwa Sekta ya Utalii Kanda ya Ziwa

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

MIRADI ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali mkoani Mwanza inaenda kufungua utalii katika Kanda ya Ziwa kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali.
Hayo yamesemwa Oktoba 16,2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alipokuwa akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi, ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR eneo la Fela na uzinduzi wa jengo la huduma ya macho katika Hospitali ya Bugando.

Ametaja miradi ya kimkakati itakayosaidia kukuza utalii kuwa ni ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi, ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR katika eneo la Fela, Meli na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza.
“Tunaamini kanda ya ziwa itakuwa ni kitovu mahususi cha utalii nchini,” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amefafanua kuwa uwepo wa miradi hiyo utarahisisha usafiri kwa watalii wanaotembelea jiji hilo kutoka nchi za jirani na wakati huohuo Wizara inaendelea kupanua wigo wa utalii kupitia utalii wa mikutano na utalii wa majini.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amehamasisha wananchi hususan wa mkoa wa Mwanza kuendelea kupanda miti ili kutunza mazingira, kutunza uwepo wa hali ya hewa nzuri na kutunza vyanzo vya maji.

“Wizara ya Maliasili na Utalii ina mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anapanda miti miwili, hivyo imeanzisha vitalu vya miti ambayo itagawiwa kwa wananchi,”amesema.
Aidha, ameitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake kwa kufanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha miradi hiyo inasonga mbele.

“Tuko pamoja kuhakikisha Serikali inasonga mbele chini ya Kiongozi wetu Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Mhe. Masanja.
Ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa inaendelea Mkoani Mwanza ambapo tarehe 17 Oktoba,2022 atatembelea Kisiwa cha Ukerewe, Kisiwa cha Gana na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Stendi ya Nyegezi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news