Serikali yapandisha madaraja watumishi 262,800, Rais Samia aridhia wengine 67,00 wapandishwe

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Jenista Mhagama amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewapandisha madaraja watumishi 262,800 hadi kufikia Septemba 2022. 
 
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hadi kufikia Septemba, 2022 ameshawapandisha madaraja watumishi 262,800 ambao kwa miaka zaidi ya mitano walikuwa hawajapanda. Na kila mwezi Serikali inatumia sh. bilioni 58.3 kulipia mishahara iliyopandishwa,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana Oktoba 19, 2022 mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipopewa nafasi kuzungumza na viongozi wa mkoa, wilaya na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma kwenye kikao alichokiitisha ili kuwakumbusha watumishi wajibu wao.

“Tarehe 22 Aprili, 2021 Mheshimiwa Rais Samia alilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza na kuweka vision yake. Mheshimiwa Rais anatambua kuwa rasilmali watu ndiyo inasimamia rasilmali fedha. Na ndiyo maana Serikali inagharamia sana uendelezaji wa rasilmali watu nchini.”

Amesema katika bajeti ya mwaka 2022/2023, watumishi 120,210 wametengewa fedha ili wapandishwe madaraja. “Hii ni kutokana na ukweli kuwa tulikuwa na watumishi 67,000 wa mwaka 2015, 2016 na 2017 ambao walikuwa na barua za kupanda madaraja lakini zilifutwa na wala hawakupandishwa madaraja hayo.”

“Naomba niwahakikishie kuwa Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa hawa wote wapandishwe madaraja na kabla sijaja ziara hii, nilicheki taarifa za mfumo wa hali ya utumishi na hali ya mshahara na kukuta wote wamepandishwa madaraja ila wanatofautiana kwenye ngazi na miaka ya utumishi. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa wote wapandishwe kwa mserereko,” amesema.

Amesema kulikuwa na tatizo la watumishi kutolipwa malimbikizo ya mishahara (arrears) ambayo Mheshimiwa Rais aliamua yote yalipwe. “Kulikuwa na watumishi 113,964 ambao walikuwa wanadai arrears na tumetumia shilingi bilioni 196.68 kulipa hizo arrears.”

Aliwaeleza watumishi hao kwamba kwenye bima ya afya, Mheshimiwa Rais aliridhia kuongezwa kwa umri wa wategemezi kutoka miaka 18 hadi 21 ili kuwapunguzia mzigo watumishi wa umma.

“Sasa kama Mheshimiwa Rais anafanya hayo yote kwa ajili yetu, iweje rushwa na upotevu wa fedha viendelee kuwepo kwenye Halmashauri zetu?”, alihoji na kuwataka watumishi hao watambue kuwa haki inaenda na wajibu na heshima inarudishwa kwa heshima.

Wakati huohuo, Waziri Mhagama amesema Serikali imebadilisha muundo katika Sekretarieti za Mikoa na hivi sasa wanamtambua Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia utawala na rasilmali watu kama msimamizi wa maadili na haki za watumishi kwenye Halmashauri.

“Tumempa majukumu ya kusikiliza malalamiko na kero za watumishi, kuendesha mabaraza ya wafanyakazi lakini kubwa tumempa jukumu asimamie maadili na kuzuia mianya ya rushwa kwenye Halmashauri zetu.”

Mapema, Naibu Waziri (OR-TAMISEMI), David Silinde alisema Serikali ya awamu ya sita imeamua kujenga hospitali katika Halmashauri za Wilaya 35 ambazo hazikuwa na hospitali za wilaya ambapo katika mkoa wa Ruvuma kuna Halmashauri tano za aina hiyo.

Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Mbinga, Songea, Madaba, Nyasa na Namtumbo. "Hizi zimeshaanza kujengwa nchi nzima na tumetenga sh. bilioni 35 za kuendeleza ujenzi katika hospitali hizi."

Amesema katika mwaka huu wa fedha zahanati 700 nchini zimetengewa sh. milioni 50 kila moja ili kumalizia ujenzi wake. "Hizi ni sh. bilioni 35 nyingine na hatuna budi kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi hii ili itoe huduma kwa wananchi wetu."

Kuhusu sekta ya elimu, Naibu Waziri Silinde amesema wanafunzi milioni 1.56 wamefanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu na kwamba wizara yake inatarajia wanafunzi zaidi ya milioni 1.2 watafaulu mtihani huo.

“Ili kukabiliana na uhaba wa madarasa mwakani, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 160 za kujenga madarasa 8,000 ili wanafunzi wa kidato cha kwanza wasipate shida,” amesema.

Post a Comment

0 Comments