Tanzania yapiga hatua huduma jumuishi za fedha

NA MWANDISHI WETU

MALKIA Maxima wa Uholanzi ameipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ukuaji wa huduma jumuishi za fedha nchini ambapo idadi ya watanzania wanaopata huduma za kifedha imepanda kutoka asilimia 17 kwa mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 58 kwa mwaka 2022.
Malkia Maxima wa Uholanzi akifafanua jambo kuhusu Huduma Jumuishi za Fedha wakati wa kikao na Gavana, Prof. Florens Luoga kilichofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam leo.

Akizungumza alipokutana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga leo Oktoba 19, 2022 jijini Dar es Salaam, Malkia Maxima ambaye pia ni Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Huduma Jumuishi za Fedha amesema kuwa, pamoja na kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kifedha nchini, idadi kubwa ya watanzania bado wanafanya malipo kwa kutumia pesa taslimu hivyo kupunguza ukuaji wa malipo ya kidijitali.
“Malipo ya kidijitali yatachochea ukuaji wa biashara, kuongeza uwazi na hata kuwezesha watumiaji wa huduma za kifedha kupata mikopo kwa urahisi,”amesema.
Malkia Maxima wa Uholanzi akifafanua jambo kuhusu Huduma Jumuishi za Fedha wakati wa kikao na Gavana, Prof. Florens Luoga kilichofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam leo.

Malkia Maxima ameongeza kuwa, ili kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha hadi asilimia 100 ni muhimu kuangalia kama wateja wanamudu gharama ya huduma za kifedha, namna ya kuhusisha sekta za kiuchumi kama kilimo pamoja jinsi gani mabenki na kampuni za mawasiliano zinatumia teknolojia kuleta mabadiliko.

Awali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga alieleza kuwa BoT inatayarisha mpango wa kuendeleza utekelezaji wa huduma jumuishi za fedha unaolenga kuongeza idadi ya wananchi wanaofikiwa na huduma za fedha nchini na kwa bei rahisi.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga akielezea jambo katika kikao na Malkia Maxima wa Uholanzi kilichofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam leo.

“Benki Kuu ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo utakaohakikisha kuwa huduma jumuishi za kifedha zinapatikana kwa urahisi au bila malipo,”amesema.
Malkia Maxima wa Uholanzi (katikati) akiteta jambo na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Angellah Kairuki. 

"Kwa kushirikiana na timu maalum iliyoambatana na Malkia Maxima, kutakua na mpango wa tatu wa kuratibu jinsi gani ya kupanua wigo wakupeleka huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi,"ameeleza Gavana Luoga.

Malkia Maxima alikuja Tanzania mara ya kwanza mwaka 2010 wakati ambapo BoT inaanza mchakato wa kutekeleza huduma jumuishi za fedha. Pia alikuja 2013 na kuzindua mpango maalum wa kwanza utekelezaji wa huduma jumuishi za fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news