Serikali,wadau kuimarisha ushirikiano usimamizi wa maafa nchini

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimeti ya Maafa imeeleza itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa masuala ya maafa nchini ili kuendelea kusimamia na kuratibu masuala hayo kwa lengo la kupunguza madhara yatokanano na maafa.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Wadau wa Masuala ya Afya Moja wakifuatilia mkutano huo.
Akiwasilisha hotuba kwa niaba ya mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa wakati wa mkutano wa wadau wa masuala ya Afya Moja uliofanyika katika Ukumbi wa Edema mkoani Morogoro, Bi.Valentina Sanga alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha masuala ya maafa yanaratibiwa na kusimamiwa kwa ufanisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mratibu wa Afya Moja,Bi.Valentina Sanga akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Masuala ya Afya Moja walipokutana mkoani Morogoro kwa lengo la kujadili maendeleo ya Utekelezaji wa shughuli za Afya Moja.

Mkutano huo ulihusisha wawakilishi kutoka katika wizara mbalimbali za kisekta, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, wawakilishi kutoka katika Taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo;TAWIRI na TANAPA, na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR, Waratibu wa Dawati la Afya Moja pamoja na washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mshauri Elekezi kutoka Shirikika la Afya Duniani (WHO), Bi.Peragia Muchuruza akiwasilisha taarifa wakati wa mkutano huo.

Alieleza kuwa, kutokana na matukio ya hivi karibuni ya milipuko ya magonjwa kama vile janga la UVIKO – 19 ambalo limeathiri nchi mbalimbali duniani; yamedhihirisha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kupambana nayo. 

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na inaendelea kuimarisha mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo katika eneo la kupambana na changamoto za majanga yanayovuka mipaka na kuathiri sekta nyingi za kiuchumi na kijamii.
Afisa Ufuatialiaji wa Mwenendo wa Maradhi kutoka Zanzibar Epidemiology Disease Surveillance Unit (ZEDSU) akichangai hoja wakati wa mkutano huo,kulia ni Mratibu Miradi kutoka Taasisi ya PBA, Bi. Agnes Mushi akifuatilia.

“Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais itaendelea kuimarisha ushirikiano huu katika eneo la uratibu na usimamizi wa maafa na magonjwa ya milipuko ikiwa ni pamoja na hatari nyingine za afya kama Usugu wa vimelea vya magonjwa kwa kuzingatia dhana ya Afya Moja,”alisema Valetina.
Daktari Mkuu kutoka Idara Maendeleo ya Mifugo Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Ali Zahran akichangia jambo wakati wa mkutano huo.

Akieleza kuhusu dhana ya Dhana ya Afya Moja Valentina alisema ni nyenzo muhimu ya kiutendaji inayozingatia ushirikiano katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yanayoathiri afya ya binadamu, wanyama na mimea ili kutumia kwa ufanisi rasilimali chache zilizopo.

“Hatua hii ni muhimu katika kupambana na ongezeko la vimelea vya magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda binadamu. Hali ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na mabadiliko ya tabianchi na athari katika mazingira zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu zinazotekelezwa bila kuzingatia uhifadhi wa bionuai ikiwa ni pamoja na kilimo, ongezeko la watu, ukuaji wa miji na uvamizi wa binadamu katika makazi ya wanyamapori,”alisisitizaValetina.
Mhadhiri kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kutoka Shule ya Afya ya Jamii, Bi. Gladys Mahiti akifafanua jambo katika Mkutano huo.

Wakichangia hoja kwa wakati tofauti wajumbe kutoka Wizara ya Afya na Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano pale unapohitajika na kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa ili kuhakikisha masuala haya yanatekelezwa kwa ufasini na mikakati ya pamoja katika kudhibiti magonjwa upande wa binadamu na wanyama kwa faida ya wananchi wote.
Mtaalam wa masuala ya Afya Moja kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Dkt.Justine Assenga akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa masuala ya Afya Moja katika eneo la mifugo wakati wa mkutano huo.

Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Chakula Duniani FAO, Dkt. Elibariki Mwakapeje alisema wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuyafikia malengo yaliyopo.
Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Afya Moja wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wao wa siku mbili Mkoani Morogoro.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).

"Mkutano huu ni muhimu ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kutekeleza masuala ya Afya Moja, FAO tunatekeleza Sustainable development goals ambapo tunahakikisha hatuachi nyuma kundi lolote ikiwemo wenye ulemavu, hivyo tunaamini tutaendelea kutekeleza kupitia mfumo wa Four betters ikiwemo; better environment, better production, better nutrition and better life ili kuwa jamii salama," alisisitiza Dkt. Mwakapeje.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news