Simba SC yatinga kileleni mwa Ligi Kuu

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Ni kupitia mtanage ambao umepigwa leo Oktoba 2, 2022 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke katika jiji hilo la biashara.

Katika mtanange huo, Beki wa Yanga anayecheza kwa mkopo Dodoma Jiji ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abdallah Shaibu (Ninja) alijifunga dakika ya tano tu kuipatia Simba SC bao la kwanza.

Ni kabla ya washambuliaji, Mzambia Moses Phiri kufunga la pili dakika ya 45 na mzawa, Habib Kyombo la tatu dakika ya 85.

Ushindi huo unaifanya Simba SC kufikisha alama 13 na kupanda juu ya msimamo wa Ligi, wakiizidi alama mbili Namungo FC kutoka Ruangwa mkoani Lindi inayofuatia baada ya wote kucheza mechi tano.

Aidha,mabingwa watetezi Yanga SC ya jijini Dar es Salaam wanashuka hadi nafasi ya tatu kwa alama zao 10 za mechi nne.

Wakati huo huo, wenyeji Mtibwa Sugar wamelazimishwa sare ya 2-2 na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanange uliopigwa katika dimba la Manungu lililopo Turiani mkoani Morogoro leo Oktoba 2, 2022.

Katika mtanange huo, mabao ya Mtibwa Sugar yamefungwa na Nickson Kibabage dakika ya kwanza na Jean Papi Matore dakika ya 29.

Aidha, kwa upande wa Mbeya City kipa Farouk Shikaro alijifunga dakika ya 55 na Tariq Seif akafunga la pili katika dakika ya 65.

Post a Comment

0 Comments