Taifa linahitaji wasomi, zingatieni hilo-Mheshimiwa Minga

NA FRESHA KINASA

NAIBU Meya wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Mheshimiwa Naima Minga amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma (Musoma Technical Secondary School) iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara wanaotarajia kufanya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne kujiandaa vyema kusudi waweze kufanya vizuri ili waendelee na masomo ya kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Minga ameyasema hayo Oktoba 20, 2022 wakati akizungumza katika mahafali ya 60 yaliyofanyika shuleni hapo ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne ambapo amesema muda uliosalia wanapaswa kujipanga na kupitia yote waliyofundishwa na kuyatilia mkazo.

Amesema, taifa linahitaji wasomi watakaoendelea kuliletea maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii, hivyo amehimiza wazazi na walezi kuwasomesha watoto wao na kufuatilia maendeleo yao kitaaluma kwani elimu ndio urithi pekee usioharibika.

Pia, amewahimiza walimu wa shule hiyo kuwaandaa vyema wahitimu hao kiakili na kisaikolojia kusudi wakati wa mitihani yao wasiwe na hofu bali waone mitihani hiyo yakawaida jambo ambalo litawafanya wafanye vizuri zaidi.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Musomam Justine Manko amewapongeza walimu wa shule hiyo ya Ufundi ya Musoma kwa kuwafundisha wanafunzi hao kwa muda wote wa miaka minne, ambapo amesema, shule hiyo inategemewa na Serikali katika kutoa wanafunzi wenye matokeo mazuri zaidi kwani imekuwa ikiuletea sifa Mkoa wa Mara kwa kupata matokeo mazuri.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma, Magita Gabriel amesema shule hiyo ni ya wavulana ina kidato cha kwanza mpaka cha sita ikiwa na wanafunzi 1,076 ambapo kati yao 553 wanaosoma masomo ya ufundi, sayansi,lugha, na TEHAMA ni kidato cha kwanza.

Ambapo wanafunzi wa kidato cha V-VI 523 wenye tahasusi za masomo ya Sayansi na Sayansi ya Jamii wanasoma masomo ya Sayansi yaani PCB, CBG, PGM, EGM, HGE, HGK, HKL.

Huku wanafunzi 124 ni wenye ulemavu wa aina mbalimbali wakiwemo viziwi, viungo, ngozi, uoni hafifu na usonji na ina jumla ya walimu 64.

"Tunahitaji vyumba vya madarasa 29 vilivyopo ni 23 na upungufu ni tisa, tuna uhitaji wa maktaba mbili, iliyopo ni moja na upungufu ni moja, nyumba za watumishi mahitaji ni 80 zilizopo ni 23 na upungufu ni nyumba 57, pia samani viti na meza mahitaji ni 1,076, vilivyopo ni 1,006 na mahitaji ni 70, mabweni mahitaji ni 11 yaliyopo ni tisa, upungufu ni mabweni mawili, vitanda mahitaji ni 1076 vilivyopo ni 974, na upungufu ni 102,"amesema Mwalimu Gabriel.

Ameongeza kuwa, shule hiyo imekuwa ikipata matokeo mazuri ambapo kwa mwaka 2020 matokeo ya kidato cha pili daraja la kwanza walikuwa ni 96, daraja la pili 9, daraja la tatu 9, daraja la nne 12 na daraja 0 wanafunzi 8. Huku matokeo ya kidato cha nne daraja la kwanza 52, daraja la pili 27, daraja la tatu 14, daraja la nne 8, na daraja 0 wanafunzi 5.
Na kwa kidato cha sita daraja la kwanza 12, daraja la pili 87, daraja la tatu 89, daraja la nne 13 na daraja 0 mwanafunzi 1.

Kwa mwaka 2021 kidato cha pili daraja la kwanza 90, daraja la pili 13, daraja la tatu 7, daraja la nne 12, daraja la O mwanafunzi 1. Huku matokeo ya kidato cha nne daraja la kwanza 76, daraja la pili 13, daraja la tatu 12, daraja la nne 9 na daraja 0 halikuwepo. Na kidato cha sita daraja la kwanza 105, daraja la pili 88, daraja la tatu 24, daraja la nne 0.

Pia, Magita ameomba Serikali isaidie upatikanaji wa vitanda 51 vya kulalia, ujenzi wa bweni moja, pamoja na kuzungushia uzio eneo la Shule hiyo kwani limekuwa likivamiwa na wananchi wanaotaka kufanya makazi na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Aidha, amemshukuru Rais Samia Hassan kwa kutoa fedha shilingi milioni 112 kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya ufundi na shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili na samani zake ambavyo tayari vinatumika tangu shule iliyofunguliwa Januari 2022.

Awali akisoma risala ya wahitimu hao William Manga amesema kuwa, wanafunzi hao walianza wakiwa 138 ambapo waliohitimu ni 118 na wengine 20 walihama kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na sababu za kiafya na mazingira.
Amesema mbali na kusoma masomo kwa muda wa miaka minne, wameweza pia kujifunza stadi za maisha shuleni hapo ikiwemo kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa nguruwe, nidhamu pamoja na malezi ya kiroho kutoka kwa viongozi wa dini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news