Halmashauri ya Karatu yatoa rai kwa viongozi wa dini, jamii kuhusu Ebola

NA SOPHIA FUNDI

SERIKALI wilayani Karatu Mkoa wa Arusha imewaomba viongozi wa dini,viongozi wa jamii pamoja na wadau wa afya kutoa elimu kwa jamii ikiwemo kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Ebola ulioripotiwa kuingia nchi jirani ya Uganda
Rai hiyo imetolewa na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Faraja Msigwa katika Kikao cha Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi Wilaya (DPHC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri na kushirikisha wadau wa afya,baadhi ya wakuu wa idara,viongozi wa dini na mila.

Faraja amewaomba viongozi hao wakiwa kwenye maeneo yao ya ibada, kwenye mkusanyiko wowote watoe elimu ya ugonjwa huo ambao uko nchi jirani.
"Ndugu zangu ugonjwa huu kwa Tanzania bado haujaingia tunachofanya sisi kama Serikali kwa kushirikiana nanyi ni kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kukabiliana nao kama tulivyofanya kwa magonjwa mengine ikiwemo Corona,hivyo nawaomba mkiwa kwenye maeneo yenu mtusaidie, Serikali yenyewe haitaweza,"amesema Faraja.

Akitoa elimu kwa Kamati hiyo, Mganga Mkuu wa wilaya, Dkt.Lucas Kazingo amesema kuwa, ugonjwa huo hauna tiba maalum wala chanjo, kwani mgonjwa hupewa tiba saidizi kulingana na dalili alizonazo kama vile kushusha homa na maumivu.
Amefafanua kuwa, ugonjwa huo husababishwa na virusi vya Ebola ambavyo hubebwa na wanyama kama vile nyani,popo, swala na wengineo ambapo husambazwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa kula nyama,mizoga au kuwagusa.

Dkt.Kazingo amesema kuwa, ugonjwa huenezwa kupitia sehemu za wazi za mwili kama vile pua,masikio na macho ambapo humwathiri binadamu na wanyama endapo vimelea vitaingia katika mzunguko wa damu.
Amewaomba wananchi kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono au kukumbatiana, kutogusa damu, matapishi, mkojo, kinyesi, kamasi, mate, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Post a Comment

0 Comments