'Tufanye kazi kwa juhudi zote kwa sasa, hakuna ajuaye kama kesho atakuwepo maana kesho si yetu mali'

NA ADELADIUS MAKWEGA

USIKU wa Jumapili ya Oktoba 16, 2022 nililala mapema sana kutokana na kufanya kazi kadhaa ambapo ratiba yangu imebadilika kwa majuma mawili sasa, kwa kuwa nilikuwa nimechoka sana usingizi ulinijia mapema na kulala fofofo.
Afisa Utamaduni, Bw.Christopher Mhongole anayemwakilisha Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika (katikati) akitoa maelezo ya utekelezaji wa Programu kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo wakati huo, Dkt.Ally Possi (wa kwanza kushoto) alipotembelea Ofisi ya Programu hiyo Jijini Dar es Salaam, wa kwanza kulia ni alikuwa ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Urithi wa Utamaduni na Maadili ya Taifa kutoka Wizara ya Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw.Boniface Kadili.

Msomaji wangu unaweza kujiuliza au mwanakwetu alikuwa amekunywa yale maji yenye rangi ya dhahabu? Nikuume sikio kuwa hilo binafsi sijajaliwa kabisa kujaribu na wala hekima zake sizifahamu kabisa.ukitaka ushahidi uliza wale niliojaliwa kukaa nao karibu.

Nikiwa nimelala usingizi huo wa uchovu majira ya saa nane ya usiku niliamka hapa kwetu Mbagala, nilisikia sauti ya Kunguru wakilia koo, kooo, koooo…Kwa kuwa usingizi ulikatika na mie kuwa macho kwa muda mrefu masikio yangu yalikuwa tajiri wa kila kelele iliyotoka nje ya nyumbani kwetu, mara nilisikia milio ya sauti za ndege zikielekea na kuondoka uwanja wa ndenge wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Nikiwa katika kitanda cha urithi cha babu yangu kilichobadilishwa shuka na chandarua pekee, kitanda cha miaka mingi sana kikinizidi umri mara mbili, kitanda hiki kilinipa utajiri wa kumbukumbu kadhaa. 

Kwanza nilikumbuka kuwa kuna wakati fulani, watumishi fulani walitembelea Mkoa wa Iringa, walifika hapo na kufanya mafunzo yao vizuri sana. 

Siku za mwishoni mwa juma walikuwa wakitembelea maeneo maarufu ya mji huu. Wikiendi ya kwanza waliamua kwenda pahala lilipo fuvu la Chifu Mkwawa na siku hiyo iliishia huko.

Juma lingine walikubaliana watembelee vyuo vikuu kadhaa vya Iringa ambavyo ni Chuo Kikuu cha Mkwawa, Chuo Kikuu cha Ruaha na Chuo Kikuu cha Iringa. Kwa kuwa watumishi hao wapo baadhi yao walisoma katika vyuo hivyo, huku wengine wakisoma vyuo vingine hadi ughaibuni, safari hii ya vyuo vikuu walitamani kuona vyuo walivyosoma wenzao ili kulingansiha na vyuo vyao walivyosoma huko ughaibuni.

Wakaingia katika gari hadi katika chuo kikuu kimojawapo, walipofika hapo walikuta chuo kimetulia sana na kwa bahati nzuri mlinzi aliwapokea vizuri sana, akawauliza mna shida gani?.

Ndugu hawa wakamueleza kuwa wao walisoma hapo chuoni wamekwenda kutembea, wakaulizwa je? Mliwasiliana na chuo juu ya ugeni huu? Wakajibu hapana bali wamekwenda kutembelea chuo hiki kwa kuwa wapo Iringa.

Mlinzi akawauliza nyinyi wote mmesoma hapa, ndugu hawa wakajibu ndiyo, wakati siyo kweli, mlinzi akacheka sana halafu akakataa kuwaruhusu kuingia chuoni hapo. “Kama mngekuwa mmewajulishwa hawa wenye chuo mapema ningewaruhusu kuingia.”

Mlinzi huyu alirudi katika kibanda chake na kuwaacha ndugu hawa wanashangaa na safari ya kuzungukia vyuo vikuu ilishia hapo hapo, haikuendelea tena.

Wakageuza gari lao na kuanza kurudi walipofikia. Wakiwa ndani ya gari hilo wengine wakisema huyu mlinzi ana shida, wengine wakisema huo ndiyo ukweli.

Wengine wakitania kuwa wale waliosoma chuo hiki walikuwa hawafahamiki hata kidogo? Jamaa hawa kila mmoja akifanya hukumu la tukio hilo kivyake kivyake, lakini ukweli unabaki walikataliwa.

Kumbuka msomaji wagu nipo kitandani nalikumbuka tukio hilo la wasomi hawa, Mwanakwetu nikapitiwa na usingizi mzito, usingizi huu ulikuja vizuri mno na nikalala kwa muda kidogo, azana ya kwanza iliniamsha tena, nikawa macho kwa muda kidogo, kwa kuwa tukio hilo la jamaa hawa waliokataliwa kuingia chuoni lilitokea Iringa na mmojawapo wa walikuwamo humo ni malimu mwezangu niliyewahi kusomesha naye huko Iringa Vijijini, hapo hapo nilimkumbuka mwalimu huyo na mwanafunzi wetu mmoja anayefahamika kama Christopher Mhongole, huyu ni mhehe wa Isimani Iringa Vijijini.

Tulimfundisha mwaka 2004/2005 Shule ya Sekondari Isimani. Kwa sasa ndugu Mhongole ni Afisa wa Programu ya Urithi wa Ukombozi, jijini Dar es Salaam. Mwaka 2004/ 2005 ndugu Mhongole alikuwa Kaka Mkuu wa shule ya Sekondari Isimani, nakumbuka shule hii wakati huo ilikuwa inapokea misaada mingi kutoka taasisi mojawapo ya Italia vikiwamo vitabu na misaada mingine kadhaa kupitia Kanisa Katoliki la Mtakatifu Karoli Luwanga Parokia ya Isimani. 

Hata wanafunzi na walimu wa shule hii walipa hisani ya kujisomea bure katika maktaba ya parokia hii, binafsi nikiingia katika maktaba hiyo mara kadhaa.

Nikiwa mwalimu hapo shuleni siku moja nilipewa kazi na Mkuu wa Shule kusimamia zoezi la kupokea vitabu na kuviingiza ofisini kutoka kwa wageni hao walivyokabidhi katika hafla fupi. 

Kazi hiyo tulisaidiana kuisimamia, wakati huo mwanakwetu nikiwa mwalimu kijana sana na ndugu Mhongole (Kaka Mkuu) akiwa na yeye kijana mdogo, mtulivu mno, mkimya sana lakini ni mchapa kazi sana. 

Wakati wa zoezi hilo linaendelea, niliona kitabu kimoja kilichokuwa kama Encylopedia Britanica kilikuwa na maelezo katika lugha ya Kiingereza, kitabu hiki kilikuwa kikiyanukuu baadhi ya maneno yaliyosemwa na watu maarufu na kuyaelezea kwa kina, mojawapo ya nukuu hii ilikuwa ni hii;

“Mwabudu Mungu kama unakufa kesho;Fanya kazi kama utaishi milele.”

Kitabu hiki kilieleza kuwa haya ni mojawapo ya simulizi mashuhuri za dini ya Kiisilamu. Ukiweka kando umashuhuri wake binafsi ilinivutia sana kwa kuwa ilihimiza mambo makubwa mawili kwa wakati mmoja; kwanza kumuabudu Mungu na pili kufanya kazi kwa bidii.

Nikiwa nakisoma nikasema mtu anayefanya kazi kwa bidi na huku akitambua anaweza kuondoka hapo alipo muda wowote ule hawezi kupoteza muda wake kwa mambo yasiyofaa, atalenga kuyakamilisha mambo haya muhimu kwa wakati sahihi, akifahamu kuwa kama akilala je anaweza kuamka?

Kumbuka msomaji wangu nipo kitandani nimelala. Je wewe mwanakwetu ukirudi pahala ulipokuwapo, ulipowahi kuishi je utakumbukwa kwa mema, je uliokaa nao watakutambua? Je wataona fahari uwepo wako? Au watakukataa?.

Inawezekana mwanakwetu alikutana na kaka wakuu wengi katika maisha yake ya ualimu, lakini hata majina yao hayakumbuki, kwa nini analikumbuka jina la Christopher Mhongole?.

Kwa hiyo tukipewa nafasi yoyote ile tunawajibu mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii zote ili tusijilaumu, tusije kukakataliwa na wale tuliofanya nao kazi au wale tuliokuwa tunawafanyia kazi, tunapaswa kuishi kwa kumkumbuka Mungu na kufanya kazi kwa juhudi zote.

Mwanakwetu naomba niishie hapo, naiweka kalamu yangu chini kwa kusema kuwa tufanye kazi kwa juhudi zote kwa sasa hakuna ajuaye kama kesho atakuwepo maana kesho si yetu mali.

0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news