VIFAFIO yakoleza kasi ya elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma Mkoani Mara limetoa mafunzo kwa wajumbe ngazi ya kata wa Kamati ya Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kutoka Kata ya Bwasi na Bukumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
Shirika hilo linatekeleza mradi wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya mialo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Musoma ambapo kata saba za Wilaya ya Musoma ikiwemo Bwasi na Bukumi zinanufaika na mradi huo na kata nne kutoka Wilaya ya Bunda na unafadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Sociey.

Mafunzo hayo yamefanyika Oktoba 5, 2022 katika Kijiji cha Busekera Kata ya Bukumi yakilenga kuwajengea uelewa na mbinu madhubuti za utekelezaji wa majukumu yao. Ili wawajibike kikamilifu kufanikisha malengo ya (MTAKUWWA).
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Meneja wa VIFAFIO, Majura Maingu amewataka wajumbe wa kamati hizo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika ngazi ya kata ikiwemo kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu kuimarisha ulinzi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kushiriki kutoa huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Pia Majura amewasisitiza kuandaa na kuunganisha shughuli za mpango katika ngazi za vijiji, kuratibu upatikanaji wa rasimali kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mpango kwenye vijiji na vitongoji, kuhamasisha utekelezaji wa mapango na kutoa taarifa za robo mwaka kwa ngazi ya halmashauri, kufuatilia na kuthimini utekelezaji wa mpango Katika vijiji, kuwezesha uibuaji, uandaaji na ujumuishaji wa afua na bajeti za utekelezaji wa mpango wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na watoto.
Majukumu mengine amewasisitiza kushawishi na kushauri watoa maamuzi kuzipa kipaumbele afua za ukatili dhidi ya Wanawake na watoto kwenye Mipango ya kata na vijiji, kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa mpango Katika ngazi ya kata kwa maamuzi, kuwezesha ushiriki wa Wadau wote wanaohusika na eneo la utekelezaji ili kuepuka mwingiliano wa utekelezaji wa shughuli za mpango.

Ameongeza kuwa, mpango huo ni muhimu katika kueleza wadau wa utekelezaji wa (MTAKUWWA) namna ya kuandaa kamati za kusimamia utekelezaji wa mapango katika ngazi zote na kuleta uwiano katika uanzishwaji na uendeshwaji wa kamati.

Aidha amewataka wajumbe wa kamati hizo Kuzingatia afua za 'MTAKUWWA' ikiwemo suala la kuimarisha uchumi wa kaya, mazingira salama shuleni na stadi za maisha, utoaji huduma kwa waathirika wa ukatili, malezi, kuimarisha Mahusiano na kuziwezesha familia, utekelezaji na usimamizi wa sheria, uratibu, ufuatiaji na tathimini pamoja na suala la mila na desturi.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia unaotekelezwa na Shirika hilo la VIFAFIO, Robinson Wangaso amesema kuwa, mradi huo utahusisha kutoa elimu kwa wavuvi maeneo ya mialo, kutumia michezo kutoa elimu, kufanya mikutano ya hadhara na wavuvi, kufanya Majadiliano na wadau pamoja na kuunda klabu za kupinga ukatili wa Kijinsia kwa wanafunzi wa Shule za msingi na sekondari.

Ameongeza kuwa, mradi huo unatarajia kuleta matokeo ikiwemo kuwafanya Wanawake na watoto wachukue hatua kwa kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kwa mamlaka za serikali na Jamii iwe na uwezo wa kudhibiti vitendo vya ukatili wa Kijinsia sambba na kuimarisha mfumo bora katika kamati za Vijiji na kata zinazohusika na kupinga vitendo hivyo.

Awali Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vincent John akifungua mafunzo hayo amelishukuru Shirika la VIFAFIO kwa kutekeleza mradi wa kupambana na vitendo vya ukatili maeneo ya mialo ambapo amesema Halmashauri hiyo shughuli za uvuvi zinafanyika, hivyo kupitia mradi huo utasaidia mapambano ya vitendo hivyo na kuimarisha usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya jamii na taifa pia.
Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya kata inaundwa na Afisa maendeleo ya jamii kata, tabibu, Afisa Ustawi wa Jamii, Polisi, Hakimu, mawakili wa azaki,Mratibu wa Elimu, Viongozi wa dini, vikundi vya watu wasiojiweza, watu wenye ulemavu, watu mashuhuri na wawakikishi wawili wa mabaraza ya watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news