Wahoji ni nani aliyesababisha hasara ya milioni 65/- Nachingwea?

NA DIRAMAKINI

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi wamewatupia lawama watendaji wa halmashauri hiyo kwa kusababisha halmashauri hiyo kudaiwa shilingi 65 milioni na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Wakizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, uliofanyika mjini Nachingwea, walisema wao kama madiwani walikataa mpango wa halmashauri hiyo kupitia kampuni yake ya Nachingwea Investment and Supplies Company Limited kuendesha maghala hayo badala ya mzabuni.

Walisema tangu awali walikataa mpango huo, hata hivyo wataalamu waliwashawishi kwa kuwahakikishia kwamba kampuni hiyo ingeweza kuendesha na kupata faida. Hata hivyo, hivi sasa halmashauri hiyo inadaiwa na bima kiasi cha shilingi 65,913,518.81.

Diwani wa Kata ya Mnero Ngongo, Hamis Mbinga alisema mpango wa halmashauri kuendesha maghala hayo kupitia kampuni yake waliukataa. Hata hivyo wataalamu waliwashawishi na kuwahakikishia ingepata faida.

Alisema ni jambo la kushangaza kusikia halmashauri inadaiwa kiasi hicho cha fedha kutokana na hasara iliyosababishwa na unyaufu wa korosho ghafi kwenye maghala hayo na gharama za uendeshaji.

Mbinga akiungwa mkono na madiwani wenzake alisema licha ya kukataa mpango huo, lakini pia katika kikao cha baraza lililopita wataalamu hao hao waliwaaambia madiwani kwamba hakuna hasara iliyopatikana na hakuna kampuni inayo idai halmashauri hiyo.

Mbinga pia aliitilia shaka taarifa hiyo kwamba haikuwa sahihi kwamadai kwamba haikuwa na mchangunuo wa mapato na matumizi ambao ukweli wa gharama za uendeshaji ni kubwa kiasi cha kusababisha hasara.

Diwani wa Kata ya Namikango, Omari Siasa aliungana na Mbinga kwa kusema wao kama madiwani walikataa mpango huo nakwamba walijua watapata hasara. Hata hivyo, ni kama hawakusikilizwa. Badala yake walihakikishiwa kwamba kusingekuwa na hasara.

Siasa alishauri kwamba kutokana na hasara hiyo wapo watu ambao wanasitahili kuwajibika. Kwa hiyo vyombo vya uchunguzi vichunguze ili kuwabaini watu hao na wachukuliwe hatua za kisheria. Huku Diwani wa Kata ya Namapwia, Omari Lingumbende akihoji ni nani aliyesababisha hasara na hatua gani zimechukuliwa dhidi ya mtu huyo.

Diwani wa kata ya Naipanga, Kambona alisema sababu zilizotajwa kusababisha hasara hiyo hazina nguvu. Kwani sababu ya unyaufu ilipigwa marufuku na waziri mkuu mheshimiwa Kassim Majaliwa. Kwani unyaufu unatumiwa kama njia ya watu kujinufaisha.

Alisema kauli hiyo ya waziri mkuu ni kauli ya serikali nakwamba hadi sasa agizo hilo halijatenguliwa. Hali inayo maanishwa kwamba katazo hilo bado linafanyakazi.

Kuhusu gharama za uendeshaji, diwani Kambona alisema hata sababu hiyo haikubaliki. Kwani kabla ya mpango huo kuanza kutekelezwa iliundwa timu ambayo ilikwenda katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ili kujifunza jinsi ya kuendesha maghala. Ikiwamo faida, hasara na changamoto.

"Tulisema hatuwezi kuendesha wenyewe hatukusikilizwa. Kuhusu gharama wataalamu mliziona na mkakokotoa na kuziainisha mkatuthibitishia kwamba kungekuwa na faida. Sasa mnatuambia kuna hasara na tunadaiwa shilingi milioni sitini na tano na kwamba imesababishwa na unyaufu wa korosho tani arobaini na tano na gharama za uendeshaji," Kambona alisema.

Diwani huyo wa Kata ya Naipanga aliwatupia lawama watendaji kwakusema kuna uzembe ulifanyika wa kushindwa kuwajibika kikamilifu. Kwa hiyo inatakiwa waelezwe kwanini wataalamu wameshindwa kuendesha maghala na kuamua msimu huu wa 2022/2023 yaendeshwe na mzabuni. Lakini pia waelezwe baada ya kushindwa kuendesha maghala kampuni hiyo imebuni kufanya miradi gani.

Naye Diwani wa Kata ya Mitumbati, mchungaji Simoni Njenda alisema wataalamu walifikiria faida zaidi bila kuziona changamoto. Hali ambayo ilisababisha waaminishe madiwani kwamba kusingekuwa na hasara. Lakini pia wataalamu hao wanasahau kwamba waliwahakikishia madiwani kwamba kusingekuwa na hasara.

"Wasomi kumbukumbu zenu zipo kwenye makaratasi, tusiosoma hawategemei karatasi tunahifadhi kichwani. Wasioona nao wanatunza kumbukumbu kwa njia zao. Sisi tunakumbuka mliyotuamba. Nyinyi mliona kuna faida na mkatuaminisha, nasisi tuliamini kwasababu tunawaaamini tukawa tunatembea na mawazo ya faida," Mchungaji Njenda alisisitiza.

Diwani Njenda pia licha ya kupinga sababu ya unyaufu, lakini pia alihoji korosho hizo zilikaa ghalani kwa muda gani kabla ya kuchukuliwa na wanunuzi kiasi cha kunyauka kufikia uzito wa tani 45. Kwani unanyaufu unapatikana kuanzia kipindi cha miezi sita.

Kwa upande wao wataalamu walisisitiza kwamba sababu zilizotolewa ni sahihi. Kwani makisio sio kitendo. Makisio ni nadharia nitofauti na vitendo. Kwa hiyo kilichotokea ni jambo la kawaida katika biashara.

Mkuu wa kitengo cha ukaguzi wa ndani cha halmashauri hiyo, Kenneth Mwangama alisema kuna nadharia na vitendo. Kwa hiyo kilichotokea ni mabadiliko ya kawaida. Huku akiweka wazi kwamba kampuni zilizonunua korosho katika msimu huo wa 2021/2022 zilikuwa nyingi.

Hata hivyo kampuni zilizojotokeza na kudai ni chache. Lakini pia akiwambusha madiwani kwamba taarifa na mchangunuo wa mapato na matumizi ya maghala hayo walipewa (walisomewa).

Alibainisha kwamba ingawaa uzito wa unyaufu ni tani hizo 45 ambazo thamani yake inazidi fedha zinazodaiwa. Ni kutokanana kampuni zilizojitokeza kudai ni chache. Kwa hiyo hakuna ubabaishaji wala uongo kwamba kiasi cha unyaufu ni tani 45 kama ilivyoelezewa na mtendaji mkuu wa kampuni ya Nachingwea Investment and Supplies Company Limited, Wakili Jonas Maro.

Nae mkuu wa idara ya kilimo (DAICO), Raphael Ajetu aliweka wazi kwamba unyaufu unachangiwa na baadhi ya wakulima ambao wana tabia ya kupeleka sokoni korosho zisizo kaushwa. Kwa msingi huo korosho za aina hiyo zinanyauka haraka hata kabla ya miezi sita.

Ajetu pia aliweka wazi kwamba kampuni ambazo zimelipwa na bima kufidia mzigo ambao hazikupata ni zile ambazo zilijaza fomu namba saba. Nakwamba shirika la bima ndilo lililowajulisha kiasi cha fedha zilizolipwa na kampuni zilizolipwa.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Ali Mfaume Ali Kawawa alisema yeye haungi mkono na hafurahishwi na hali iliyotokea.

Mhandisi Kawawa alisema kufuatia hali hiyo wamemuagiza mkaguzi wa ndani achunguze ili kubaini sababu za hasara hiyo. Ikibidi watavishirikisha vyombo vingine vilivyo nje ya halmashauri ili ukweli ubainike na hatua sitahiki zichukuliwe baada ya kupata ripoti ya uchunguzi huo. Maelezo ambayo yaliungwa mkono na mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye ni diwani wa Kata ya Mbondo, Adnan Mpyagila.

Kawawa pia alitoa wito kwa madiwani na wataalamu kuaminiana ili wafanye kazi kama timu moja kwa masilahi mapana ya halmashauri badala ya kulaumiana na kushutumiana. Kwani maamuzi yanayofanyika yanawashirikisha wote. Kwa hiyo yanakuwa maamuzi ya wote nasio ya upande fulani hata pale inapotokea kinyume na matarajio.

Awali mtendaji mkuu wa kampuni ya Nachingwea Investment and Supplies Company Limited, Wakili Jonas Maro kwenye taarifa aliyosoma kuhusu mradi wa uendeshaji maghala alisema shirika la bima ya taifa linaidai halmashauri hiyo shilingi 65,913,518.81 baada ya kampuni hiyo kupata hasara iliyosababishwa na gharama za uendeshaji na unyaufu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news