Surua ipo, tusaidie kuikabili-Mhe.Othman

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema mlipuko wa maradhi ya surua ni tatizo la Ulimwengu wote, bali kinachohitajika ni taarifa sahihi, uelewa, na tahadhari kwa kila upande.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo wakati akizungumza na uongozi wa Wizara ya Afya ya Zanzibar, huko Vuga Mjini Unguja, baada ya kukamilisha ziara yake Maalum katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, jijini hapa, akikagua maendeleo ya juhudi za kukabiliana na tatizo la Surua lililoibuka kwa kasi, hivi karibuni, ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa, kimantiki kasi ya maambukizo ya Surua hapa Visiwani inaonekana ni kubwa, kwa kuzingatia uhaba wa raslimali na maandalizi duni ya kukabiliana na janga hilo, bali si vyema kukuza taarifa za uwepo wa maradhi hayo, kwa nia ya kuwatishia wageni na wale wanaopanga kutembelea Zanzibar.
“Maambukizi haya siyo suala la Zanzibar na wala Wizara ya Afya pekee bali ni la ulimwengu mzima na linahitaji hima na juhudi za kila mmoja wetu ili kuweza kukabiliana nalo,”amesema Mheshimiwa Othman.

Hivyo amesema kuwa kwa sasa kunahitajika misaada ya hali na mali, sambamba na juhudi za pamoja ili kukabiliana na janga hilo, ambapo kila mmoja anawajibika kusaidia kwamujibu wa uwezo na nafasi yake.

Aidha, Mheshimiwa Othman amesisitiza umuhimu wa kujenga uelewa kwa wananchi na jamii kwa ujumla, juu ya maambukizo hayo kwa kutumia mbinu mbalimbali, zikiwemo njia za sasa za mawasiliano, huku akipongeza juhudi zinazochukuliwa na waganga na wauguzi wa hospitali hiyo, katika kukabiliana na mlipuko wa maradhi ya surua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dokta Salim Nassir Slim, ameshukuru hatua za Serikali ya Zanzibar, ikiwemo Ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, kutembelea na kuhamasisha juhudi za Madaktari kupambana na Maradhi hayo.

Akigusia juu ya mtawanyiko wa kuenea kwa maradhi hayo hapa Visiwani, Dokta Slim amezitaja Wilaya za Magharibi A na B Unguja, kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kijografia na uwezo wa kipato miongoni mwa wananchi na wakaazi wake, huku akibainisha Mkakati wa Kampeni ya Nyumba kwa Nyumba, kwa ajili ya kuwapatia Chanjo, Watoto chini ya Umri wa Miaka 5, ifikapo Novemba 10, Mwaka huu.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Zubeida Mohamed Hussein, ameeleza uzito wa kukabiliana na mlipuko wa maradhi hayo hospitalini hapo, na zaidi kutokana na uhaba wa nyenzo, uchache wa vitanda vya kulaza wagonjwa, na uelewa duni wa mazingira ya maambukizi yake, ndani na nje ya wodi.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara hiyo, takribani watu 1315 wamepata maambukizo ya ugonjwa huo wa surua unaotibika na ambao unaambukizwa na virusi, tangu ulipolipuka hapa Visiwani mnamo Julai mwaka huu; 997 kutoka Unguja, na 318 kisiwani Pemba, huku watoto wapatao nane wakiwa tayari wamefariki.
Ziara hiyo imeongozwa na Waziri wa Afya wa Zanzibar na Naibu wake, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Mhe. Hassan Khamis Hafidh; Wakurugenzi, Watendaji na Baadhi ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news