Wanahabari waonesha moyo wa shukurani kwa Rais Samia kuelekea maboresho ya sheria

NA GODFREY NNKO

WADAU wa vyombo vya habari nchini wameonesha moyo wa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Serikali yake imeonesha usikivu na hata kutoa nafasi kwa changamoto zinazoikabili taaluma hiyo zikiwemo sheria kufanyiwa kazi.
Rais Samia tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Wadau

Mwanahabari na wakili wa kujitegemea nchini, James Marenga anasema kuwa, katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria za Habari,Serikali imeonesha nia ya kufanyia kazi vipengele mbalimbali, hivyo mchakato huo utapata majibu yatakayomaliza kiu sekta ya habari.

Amesema kuwa, nia ya Serikali ni kuhakikisha mwafaka unapatikana katika Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari na wadau wa habari wamekiri kuwepo kwa nia hiyo.

“Kwa hatua hii tunaona kuwa Serikali imeonesha nia katika kuhakikisha kuwa mabadiliko yua sheria ya habari yanafanyikiwa kazi na kupata mwafaka wa vipengele vya Sheria ya Habari vyenye ukakasi inaonekana wazi,” amesema Wakili Marenga.

Wadau wa habari wamekuwa wakilenga vifungu vinavyotisha waandishi na uhai wa tasnia ya habari nchini na kwamba, sio sheria yote ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 havifai.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo, kulikuwa na sheria ya mwaka 1976 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,”amesema Marenga.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Neville Meena akielezea kuhusiana na michakato mbalimbali inayoendelea ili maboresho ya sheria za habari nchini yaweze kutekelezeka kwa wakati anasema, awamu hii kuna dhamira njema.

“Awali Serikali haikuonesha dhamira ya kushughulikua maoni ya wadau wa habari nchini, lakini katika utawala huu wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan dhamira imeoneshwa tangu mwanzo, tunaamini tutafanikiwa," anabainisha.

Meena amesema,Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 iliacha mambo ya msingi katika kukuza tasnia ya habari na badala yake ikawa ni sheria ambazo ni ngumu kutekelezwa.

Amesema, kutokana na kuwepo kwa mazingira magumu ya habari na wanahabari nchini, tasnia ya habari iliyumba kwa kiwango kikubwa.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumika. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’amesema Bw.Meena

Amesema kuwa, kuna lawama zinaelekezwa kwa vyombo vya habari kukosa weledi, moja ya changamoto inayovikabili ni kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

Meena anasema, vyombo vya habari vinashindwa kulipa mishahara kwa kuwa, watangazaji wengi hasa Serikali kwenye halmashauri,wanatoa matangazo lakini hawataki kulipa hivyo kuchangia kushuka kwa weledi kwenye vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vinalalamikiwa kukosa weledi, lakini tukumbuke kwamba wanaotoa matangazo na kushindwa kulipa, wanachangia kutengeneza tatizo.

“Wanaoongoza kutolipa ni wakurugenzi wa halmashauri, hili linachangia kuyumbisha vyombo vya habari na ndio maana tumependekeza baada ya miezi sita mtangazaji kushindwa kulipa, licha ya kukumbushwa basi afikishwe mahakamani,’’amesema.

Pia amesema, ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kutaka wadau wa habari wakutane na kuchakata mapendekezo ya sheria za habari imetimia.

“Suala la mapendekezo yote ya wadau wa habari kupita, hilo ni suala lingine. Cha msingi ni kwamba, miongoni mwa ahadi za Rais (Samia Suluhu Hassan), ikiwemo wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu, imetekelezwa.

“Sisi kama wadau wa habari tunaamini tunakwenda kufanikiwa kwa kuwa, hata Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) ana hisia chanya katika mchakato huo,’’amesema.

Balile

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile licha ya kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kuonesha dhamira njema katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini, pia amewataka waandishi wa habari nchini kuandika matatizo yanayowahusu.

Balile ameyasema hayo Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na TEF yakiangazia uchechemuzi wa sheria za habari nchini ambayo yalifunguliwa na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania,Wiebe Jakob de Boer.
Balozi de Boer alibainishwa vyombo vya habari huru ndio msingi wa kuibua mijadala mizito na hutoa mwongozo katika utungaji wa sheria na mwelekeo chanya wa taifa.

Amesema, uhuru wa vyombo vya habari ndio moyo wa demokrasia ya nchi yoyote kwa kuwa, hutoa mwanga na mwelekeo wa taifa.

Balozi huyo amesema, mamlaka zikijenga tabia ya kusikiliza sauti za watu wote na kuchukua mawazo kwa kiwango kikubwa, itasaidia katika kufanya uamuzi wenye manufaa kwa wananchi na taifa.

‘‘Tunaamini kwamba, uwepo wa tabia ya kusikiliza sauti zote na kusikiliza mawazo ya kila mtu, inawezesha kufanya uamuzi wenye busara kwa manufaa ya taifa sambamba na kuinua maisha ya wananchi wote,’’ alisema Balozi Boer.

Kwenye semina hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatius Balile alimueleza Balozi Boer utayari wa serikali katika safari ya mabadiliko ya sheria ya habari.

Alisema, mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unahusisha taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jamii Forums.

Mbali na hayo Balile aliendelea kufafanua kuwa, "Waandishi wa Afrika katika mafunzo wanayopewa, wanapewa mafundisho kwenye vyuo na vyumba vya habari kwa ajili ya kutetea jamii, lakini katika mafundisho hayo hakuna ndani ya mtaala sehemu inayomwambia mwandishi wa habari na wewe ni sehemu ya jamii.

"Kwa hiyo, wakati mwingine wanakuwa wakijua kwamba wanafanya hiki kitu si kwa ajili ya kujitetea wao, maslahi yao, wanajua kwamba wao wanatetea jamii. Kwa hiyo hii imekuwa ni hivyo, muda wote na matatizo mengi yanakuwa kwenye vyumba vya habari, waandishi wa habari wanapata shida nyingi bila kujua na wao kumbe wanastahili kutetea haki zao.

"Ndio maana sisi kama Jukwaa la Wahariri Tanzania, tukasema huu mkondo tusipoanza kutetea haki zetu tutaendelea kuwa katika hali ngumu, mtaona kuna mashirika mengi hata yanayoteta hata zile haki za waandishi wa habari hayafanywi kazi za habari.
"Yaani unakuta shirika limeanzishwa huko mbali kabisa, halina hata ujuzi wa vyombo vya habari vinafanyaje kazi. Sisi ndio tunaovaa viatu, tunajua wapi kinabana zaidi, kwa hiyo kwa kujua matatizo yetu tukaanza kuyasemea, kuyatetea itaifanya Dunia itambue. Lakini pia tukiondoa ile kasumba hatuandiki habari zinazotuhusu.

"Kwa hiyo, umefika wakati sasa na sisi ni wanajamii na sisi tunahitaji kuishi na sisi tunahitaji kuishi na kuwa maisha bora ili tutetee haki zetu zipatikane tukiwa na hali nzuri tutasimama vyema kutetea haki za wengine kwa ufasaha.

...Vyombo vya habari vinafanya kazi ya kujenga uelewa katika jamii ili kuwafanya wananchi wafanye uamuzi kutokana na uelewa walionao.

"Watafanya uamuzi wakijua kwamba wanamtaka fulani si kwa sababu amewapa kanga au amewapa kofia ama kitenge wakati wa kampeni, lakini ameahidi kujenga miundombinu, kukuza mfumo wa elimu, kukuza uchumi. Jambo ambalo litasaidia si tu mtu mmoja mmoja bali kizazi na taifa kwa ujumla," amesema Balile.

Makunga

Kwa upande wake mwenyekiti wa zamani wa TEF, Theophili Makunga amesema, suala la utashi wa kisiasa ni muhimu katika uandishi wa sheria kwa sababu linatoa mwelekeo wa sheria husika.

"Ikumbukwe kwamba tumetoka mbali kwenye sheria ya waandishi wa habari, kwa muda mrefu nchi yetu ilikuwa inaongozwa na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, sheria ya magazeti ilikuwa na vipengele vingi sana vilivyokuwa vinambana mwandishi wa habari.

"Lakini kulingana na teknolojia iliyokuwepo wakati ule, baada ya Media Service Act, 2016 kufuta ile Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 vile vile kuna vipengele bado vinambana mwandishi wa habari.

"Lakini tunashukuru kwamba, Serikali imeliona hilo na imekubali kuongea na vyombo vya habari kurekebisha baadhi ya vipengele ambavyo tunafikiri vinawabana waandishi wa habari,"amesema Makunga.

Balile tena

Katika mwendelezo wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile anasema vyombo vya habari vinapaswa kujenga tabia ya kuanzisha mijadala yenye kuchochea ukuaji wa uchumi na sio mijadala isiyo na tija kwa nchi na wananchi wake.

Anasema, ni vema masuala ambayo yanahusu uboreshaji wa viwanda, miundombinu na kilimo ambayo yatabadilisha maisha ya Watanzania wote kutoka katika umasikini kupewa kipaumbele na nafasi zaidi kuliko zile za maisha binafsi ya watu na malumbano ambayo hayana tija.

“Kwa wenzetu katika nchi zinazoendelea wanajadili namna ya kukuza biashara na viwanda vyao kwa kuzalisha bidhaa bora pamoja na kutafuta masoko, sisi hapa tuna viwanda, uzalishaji wa gesi, lakini hauoni mijadala mingi kwenye eneo hilo, wanahabari tubadilike,”anasema Balile.

Pia amesema, wataendelea kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya sheria zinazogusa tasnia ya habari kwa kushirikiana na wadau wengine nchini.

“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayotukabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema.

Mhariri Mkuu wa Gazeti la Guardian,Walace Maugo ametumia nafasi hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kupigania haki za Watanzania na kuboresha maisha yao kupitia taaluma yao na kazi wanazozifanya kila siku.

“Kama tunavyofahamu kwamba sisi ndiyo tunaotengeneza mijadala kwenye jamii, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha maisha bora yanapatikana na watu wanafurahia maisha katika nchi yao, tusijione wanyonge kuna hatua kubwa zimechukuliwa kutokana na kazi tunazozifanya,” amesema Maugo.
Naye Neville Meena anasema, waandishi wa habari wana wigo mpana wa kufikisha taarifa zao na kuifanya jamii ichukue hatua au ishinikize hatua zichukuliwe kulingana na kile walichokisoma, kukisikia au kukiona.

Ameyasema hayo wakati akizungumzia umuhimu wa wanahabari kuchochea maendeleo, uzalishaji mali na mabadiliko ya sheria kwenye warsha ya kuwajengea uwezo wahariri kuandika na kupitia habari za uchechemuzi wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari.

“Leo hii mitandao ya kijamii na katuni zimekuwa zikitumika kufikisha ujumbe kwa jamii na kuleta mabadiliko makubwa, cha msingi ni lazima sheria ziweke misingi imara ya Watanzania kuwa na uhuru wa kujieleza, kupata habari na kusambaza,” amesema Meena.

Mhariri wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrisa amesema, jamii inapaswa iendelee kupigia kelele kwa kushirikiana na vyombo vya habari juu ya marekebisho ya sheria zinazokwaza uhuru wa habari.

Kwa upande wake, Tumaini Mbibo amesema, watu wanaweza kudhani sheria ni mbaya, lakini kumbe hawazijui hivyo jambo la msingi ni kuwawezesha wazijue ili wasizivunje na kuingilia haki za watu wengine.
“Hatuwezi kudai mabadiliko ya sheria kama hatuzijui, tufanye uzengezi wa mabadiliko ya sheria tunazozilalamikia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili tupate matokeo chanya,”amesema Mbibo.

Pia amesema, ni muhimu kwa waandishi wa habari kujua kiini cha matatizo yanayolikabili Taifa na njia za kutumia ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo husika.

Amesema, haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia, hivyo uwepo wa sheria zinazominya tasnia ya habari zinakwamisha maendeleo huku akishauri ni vema ikafanyika mipango ya kufanya ushawishi wa mabadiliko.

Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim amesema kuwa, mwandishi wa habari akijua haki zake, sheria zinazoongoza tasnia ya habari ataweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wabunge na kuwashawishi juu ya sheria zinaminya uhuru wa habari na haki za binadamu.

“Bado waandishi hatujawa na uelewa mpana wa sheria zinazotuhusu, tufanye jitihada kuzijua. Tuwashawishi wenzetu juu ya sheria zinazokwaza ukuaji wa tasnia ya habari na maendeleo ya Taifa,” amesema.

Kwa upande wake, Sylvester Hanga amesema, waandishi wa habari wanataka sheria za masuala ya habari ziwe rafiki ili zichochee demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa.

Joyce Shebe amesema, anaamini wahariri wakijua namna ya kushawishi watunga sheria, sera na mipango ya Taifa watakuwa kwenye nafasi njema ya kuchochea maendeleo ya mtu mmoja na Taifa.

Waziri Nape

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewahakikishia wadau wa habari kuwa, Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari nchini hayatapelekwa bungeni bila pande zote kukubaliana na kuridhika.

Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye ameyasema hayo Agosti 26, 2022 katika mjadala wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC ambao uliangazia kuhusu mapendekezo hayo.

"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Alifafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.

"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana.

"Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona, kwa hiyo Serikali ipo tayari, kikao cha kwanza kimeenda vizuri na nimeridhika,sasa tutakwenda kikao cha pili ambacho nitalazimika kwenda mwenyewe tukae pamoja tuzungumze tujenge hoja, wanawaza nini, tunawaza nini mwishowe tutakubaliana, nchi ni yetu wote,"alisema Mheshimiwa Nape.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news