NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.
Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo tarehe 26 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Serikali ya Misri kwa kuendelea kuthamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Tanzania hususan kwenye sekta ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama afya, elimu, maji, nishati na ujenzi wa miundombinu.
Amesema, ni kutokana na kuthamini mchango unaotolewa na Misri kwenye sekta mbalimbali za maendeleo nchini Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara nchini humo mwezi Novemba 2021 na maeneo mbalimbali ya ushirikiano yalijadiliwa na kukubalika.
“Ninayo furaha kukukaribisha nchini Mhe. Waziri. Nakiri kupokea ujumbe huu muhimu kutoka kwa Waziri mwenzangu. Nitaupitia na kuufanyia kazi na kuwasilisha kwenu mrejesho haraka iwezekanavyo,”amesema Mhe. Dkt. Tax.
Naye, Mhe. Issa amempongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa katika wadhifa huo mpya na kumweleza utayari wa Serikali ya Misri katika kushirikiana naye.
Kadhalika amesema, Serikali ya Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya pamoja ambayo nchi hizo zimekubaliana ukiwemo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere.
Pia Mhe. Issa alitumia nafasi hiyo kuikaribisha Tanzania kushirki kwenye Mkutano wa 27 wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika mwezi Novemba 2022 katika Mji wa Sharm El Sheikh, nchini humo.