BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 49

NA WILLIAM BOMBBOM

Ilipoishia...Ushindi wa kuchoma na kusambaratisha kambi hiyo ulinipa nguvu zaidi ya kuendelea na ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Mawazo yote haya yalinijia kichwani mwangu nikiwa ndani ya uvungu wa vidole vya BUNDI WA GAMBOSHI tukiwa hewani tukielekea kambini kwetu.

Endelea..

Hatimaye tulienda kutua kwenye viunga vya kambi yetu ya kichawi pale majengo, niliachana haraka na yule bundi nikaelekea kwenye jengo litumikalo kwa vikao vya kichawi.

Tayari ilikuwa ni saa tisa kasoro, niliingia ukumbini humo na kuwakuta wachawi wenzangu wakinisubiria.

Baada ya kuingia tu zililipuka shangwe, nderemo na vifijo. Kwa kiasi kikubwa kambi nzima ilikuwa imefurahishwa na ushindi wetu dhidi ya kambi ya Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Mpaka hapo kila mmoja alikuwa akiamini katika nguvu nilizokuwa nazo za kichawi. Hakuna mchawi aliyethubutu kuleta jeuri katika kambi. kama nimefanikiwa kuisambaratisha kambi nguli, kwa mtu mmoja ingekuwa rahisi.

Baada ya zogo hilo la furaha niliwaeleza wachawi hao mpango niliokuwa nao kuhusiana na ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Kila mmoja alishauri mawazo yake na hatimaye kikao kilikubaliana kuwa usiku uliokuwa ukifuata ndiyo tungeanza ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Pia tuliutumia muda huo kumchukua kafara wetu yule mbunge, tulimpeleka kwenye eneo la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA kama ilivyokuwa imekusudiwa.

Huyu ni mmoja wa wabunge waliokuwa wakilinyonya Taifa, wabunge wa namna hii wapo wengi mjengoni.

Tulimvua nguo zote mbunge huyo kisha tukajiandaa kumchinja. Kulingana na sheria za kafara,THE BOMBOM ndiye nilikuwa nikihusika na uchinjaji.

Nilichukua jambia kisha nikaanza kulipitisha shingoni mwake, damu zilikuwa zikichuruzika mfano wa maji ya bomba. Kwetu ilikuwa ni furaha maana tulikuwa tukitimiza maelekezo ya namna ya kutambikia ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Wakati damu ya mbunge huyo ikizidi kuchuruzika ardhini, alitua ndege aina ya mbayuwayu akitokea tusikojua.

Alikuwa na rangi nyeusi tii kuzidi ile ya mbayuwayu mwenyewe. Miguuni alikuwa kavaa cheni yenye alama ya mkuu wetu, tukatambua kuwa kafara yetu ilikuwa imekubalika machoni mwa mkuu wetu.

Ndege huyo alikuwa mwakilishi mwema toka kwa mkuu wa giza. Ndege huyo alikunywa damu ya kafara wetu yote, baada ya hapo alielekea kila kona ya eneo tulilokuwa tumeandaa kwa msingi wa wajengo, alitema vitu vyeusi na kuvifunika kwa kucha zake. Kitendo hiki kilifanyika haraka tena kwa umakini mkubwa, baada ya muda mchache ndege huyo alikamilisha Shughuli yake akatuaga kisha akaondoka.

Tulirudi kambini kwetu kwa miguu kwa kuwa haikuwa mbali, baadhi ya wachawi walirudi makwao na wengine waliojiamini zaidi waliendelea na shughuli zao. Niliutumia muda huo kwenda kupumzika kwenye jumba langu la mkuu wa wachawi.

Nikiwa chumbani mle bado nafsi ilinisuta, fundo la moyo lilikuwa likiniuma hasa nikikumbuka kuponyoka kwa mama yangu mzazi kila ninapomuingiza kwenye kumi na nane zangu.

Nilijiuliza maswali kadha wa kadha ambayo hayakupata majibu. Niliendelea kulala kitandani hapo huku usingizi ukiningemerea taratibu, hatimaye macho yakawa mazito kisha nikatopea kwenye lindi la usingizi.

Mara nyingi wachawi huwa tunatumia muda mfupi sana kulala. Ndugu msomaji hebu fikiria nimelala saa kumi kasoro kisha saa kumi na mbili tayari nilikuwa nimeamka. Nilifanya shughuli zangu kama ilivyo ada, taarifa za siku zao kambi zilikuwa mbele yangu.

Niliziagiza kwa mkuu wetu wa giza kama ilivyo kawaida. Baada ya hapo tuliendelea kuandaa madawa kwa ajili ya shughuli iliyokuwa mbele yetu.

Walitakiwa mafundi na vibarua wa kutosha katika kazi hiyo. Hata hivyo tulikuwa tumekubaliana kwenda kuchukua magari ya mchanga tani 30.

Magari hayo yalikuwa ni mali ya Kampuni la ujenzi wa mabwawa ya samaki liitwalo English smelters & construction. Kampuni hilo lilikuwa limepewa tenda ya kupanua kingo za *Ziwa Sagara* lilopo mji wa Itebula.

Kampuni hilo lilikuwa na magari ya aina mbalimbali yanayoshughulika na kazi za namna hiyo. Yapo yaliyotumika kubeba mchanga, kokoto na mawe.

Mengine yalitumika kubeba maji na vitu vingine, yapo yaliyokuwa yakishughulika na uchimbaji kama vile Greda, ksaveta nk.

Katika mipango yetu tukawa tumepanga kutumia vifaa vya kampuni hilo kufanyia kazi yetu ya ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Hapa nizungumze kidogo, ndugu msomaji kuna kipindi wachawi huwa tunatumia vifaa vya wanajamii kufanyia shughuli zetu.

Mfano wakati mwingine tunaweza kuchukua trekta za watu kulimia mashamba yetu, na mhusika wa trekta hilo ndiye huwa anahusika katika kazi hiyo pasipo kujijua.

Muda mwingine huwa tunatumia wanyama kulima, kama tumegundua mifugo wetu wanapaswa kupumzika huwa tunachukua ng'ombe wa sehemu yeyote.

Tuliendelea kufanya maandalizi ya kazi iliyokuwa mbele yetu kwa usiku huo. Hatimaye siku ya kuanza ujenzi wa GAMBOSHI MPYA ilikuwa imefika.

Sikuwa nikiamini macho yangu,THE BOMBOM kusimamia ujenzi wa kambi hiyo ilikuwa ni heshima kubwa sana kwangu.

Kwa muda mchache wa utumishi wangu wa kichawi katika kambi hiyo ya majengo nilikuwa nimefanya mambo makubwa.

Yote hii ni imani ya mkuu wetu wa giza kuniamini mie msukule THE BOMBOM. Wachawi wenzangu walikuwa wakiniheshimu kupita maelezo, nguvu za madawa nilizokuwanazo mwilini mwangu ziliwafanya kuniogopa.

Jioni ya saa kumi na mbili niliwaagiza wachawi wenzangu kumwaga dawa mji mzima. Walimwaga dawa kuanzia mji wa Majengo, Kigamboni, Bweru, Nguruka, Nyangabo, Lugongoni zote, Itebula, Kamfuba na Mhamakalonga.

Dawa hiyo ilikuwa na kazi ya kuwalazimisha watu kulala mapema, kila mtu ambaye angeingia katika miji hiyo ni lazima angelala mapema.

Walifanya hiyo kazi mpaka muda wa saa mbili za usiku, baada ya hapo waliwachukua wale wachina wakawapeleka kwenye lile kampuni la uchimbaji wa mabwawa.

Wachina hao walikabidhiwa yale magari wakayaendesha hadi kwenye eneo la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Hapa niseme kidogo, kanuni mojawapo ya kichawi ni kupiga kelele za juu sana kadri wanavyofanya kazi zao, wanapozungumza huwa wanatoa sauti kubwa sana.

Hii ndiyo kanuni ya dawa za kujificha, mara nyingi huwa zinaenda kinyume na ule utaratibu wa binadamu wa kawaida.

Mfano binadamu hufanya kazi mara nyingi mchana, ila wachawi hufanya usiku. Binadamu wa kawaida huwa anakula kwa kutumia vidole vyake kama kawaida, lakini misukule viganja vyao vimejikunja kinyume cha binadamu wa kawaida.

Binadamu wa kawaida huzungumza kwa sauti ya wastani, lakini misukule na wachawi huzungumza kwa sauti ya juu sana.

Ilipofika saa tatu za usiku tayari wale wachina walikuwa wameshaleta chombo cha kuchanganyia zege. greda na lori za kubebea vitu zilikuwepo, kreni ya kupandisha vitu tulikuwa tumeichukua bandarini.

Tukautumia muda huo kusomba mafundi toka mtaani. Hapa niseme kidogo, wachawi hutumia dawa tofauti tofauti kumchukua mtu kutegemea na malengo yao.

Kama ni kwenda kumfanyisha kazi mtu huyo, dawa ambazo hutumika huwa za kawaida sana. Maana kutumia dawa kali ni kumfanya mtu huyo kutokubalika ndani ya jamii yake.

Tunapokwenda kumchukua mtu kwa ajili ya kazi huwa tunatumia dawa fulani inayokuwa ndani ya kiboko siyo dawa kali.

Tunapoingia ndani ya nyumba yake huwa tunafanya manuizi fulani kisha tunamchapa kiboko hicho. Baada ya hapo mtu huyo huamka na kupita kwenye ukuta na kwenda moja kwa moja eneo la kazi.

Huenda kwa miguu japo mwendo wake huwa umechanganywa na upepo ndiyo maana huwahi kufika eneo husika.

Tulifanya hivyo kwa mafundi mwashi wote wa miji hiyo tuliokuwa tumewakusudia, punde si punde eneo la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA lilikuwa limetapakaa mafundi wakifanya kazi kwa nguvu te. Wachina misukule ndiyo walisimamia tafsiri ya michoro ya majengo, kazi ilifanyika haraka kuliko maelezo na kwa ufanisi.

Misingi ya majengo iliendelea kusimama huku zege zikimwagwa kwa ufasaha katika bimu za majengo husika.

THE BOMBOM niliyashuhudia haya yakifanyika machoni mwangu huku hali ya hewa ikiwa salama katika mazingira hayo.

Ujenzi wa misingi kadha wa kadha ya majengo hayo iliendelea kukamilika usiku huo, mafundi walikuwa wakifanya kazi kwa nguvu zote.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji ngoja nikuibie siri kidogo ya kutambua kama utakuwa umechukuliwa na wachawi kuwafanyia kazi.

Kama watakuwa wamekuchukua kwa ajili ya kukufanya kiti, mara nyingi utaamka kifua kinauma maana huwa tunawakalia mgongoni halafu upande wa nyuma ya mapaja karibu na makalio huwa panauma zaidi.

Ukiona hali hiyo tambua ulikuwa kiti kwenye kikao cha wachawi kilichofanyika eneo fulani usiku huo. Endapo utakuwa umechukuliwa kwenda kuchunga ng'ombe au wanyama wengine, asubuhi ukijichunguza kwenye kidole chako gumba cha mguu wa kulia ndani ya kucha utakuta kuna udongo mweusi sana.

Ni vigumu kwako kulijua hilo maana kwa mbali hufanana na uchafu mweusi ndani ya kucha. Endapo utakuwa umechukuliwa kwenda kubeba mizigo, mara nyingi kiuno ndicho huuma.

Ili kutunza siri ya wewe kugundua, wachawi huwa wanahamishia maumivu ya mabegani kiunoni. Ukisikia maumivu makali kiunoni huku nyonga ikionekana kugoma, basi tambua usiku huo umebebeshwa vitu vingi.

Endapo ulichukuliwa kwa ajili ya kufundisha, maana kuna muda wachawi huwa tunawachukua walimu kwa ajili ya kufundisha misukule mambo fulani.

Hapa sauti ya mwalimu huamka ikiwa haisikiki vyema, koo lake linakuwa linauma kuliko kawaida. Hii ni dalili ya kuwa mwalimu huyo alichukuliwa kwenda kufanya kazi za kichawi.

Dalili hutofautiana kulingana na shughuli moja kwenda nyingine, mfano endapo mtu alichukuliwa kwenda kujenga majengo.

Cha kwanza yeye huletewa ndoto ya inayomuonesha kuwa anajenga jengo fulani zuri akiwa na mafundi wengine. Kimsingi hiyo huwa siyo ndoto bali ni kweli, asubuhi akiamka kitandani kwake huwa kuna mchanga mwingi. Pia katika shuka yake huwa kuna...

ZIMUHILA?
THE BOMBOM

Post a Comment

0 Comments