Waziri Mkuu atoa siku 15 kwa Mkandarasi wa barabara

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kuanzia Oktoba 20, 2022 kwa kampuni ya Inter Country Contractors kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa miradi ya barabara katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongoza kikao cha viongozi wa Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Ukerewe kuhusu ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angela Kairuki na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma Oktoba 20, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo Oktoba 20, 2022 alipokutana na Waziri wa Nchi -OR TAMISEMI, Viongozi wa Wilaya ya Ukerewe na Watendaji wa TARURA ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kuwa kampuni hiyo ilipewa kandarasi ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 13 kwa kiwango cha lami na changarawe katika kisiwa hicho ambapo ilipaswa kukamilisha kazi hiyo Julai 2022.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, katika hili tumetoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa, tunachotegemea ni uaminifu wenu na utekelezaji wa miradi hii iwe ya viwango na mkamilishe kwa wakati”

Mheshimiwa Majaliwa amesema ni vyema Mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mikoa na Wilaya wakatekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini na ukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema wamepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kuahidi kufanya mapitio makubwa ya mfumo wa kiutendaji wa TARURA ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ndani ya taasisi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news