Yanga SC na UNICEF waingia mkataba wa kihistoria kukabiliana na UVIKO-19, Ebola

NA GODFREY NNKO

KLABU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Tanzania imeingia mkataba wa miezi sita na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa ajili ya kutoa elimu na kuwapa taarifa Watanzania kuhusu UVIKO-19 na namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa wa Ebola.

Virusi vya Korona (UVIKO-19) ni kundi kubwa la virusi ambavyo kwa kawaida hupatikana kwa wanyama na husababisha maradhi hatari yanyohusiana na upumuaji kama vile Dalili za Upumuaji za Mashariki ya Kati (Middle East Respiratory Syndrome (MERS-CoV) na Dalili Kali na Hatari za Upumuaji (Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS- CoV).

Aidha,Ebola ni ugonjwa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90 ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan.

Kutokana na changamoto za magonjwa hayo ambayo yamekuwa yakidhoofisha nguvu kazi katika jamii na Taifa,Serikali, UNICEF na wadau mbalimbali wamekuwa wakitumia kila njia kutoa elimu na hamasa ili kuhakikisha jamii inayashinda magonjwa hayo hatari.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 18, 2022 Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi
Hersi Said amesema kuwa, ni furaha kubwa kwa ajili ya timu hiyo kuingia makubaliano na Shirika la Umoja wa Mataifa.

Septemba 20, 2022 Serikali ya Jamhuri ya Uganda ilitangaza mlipuko wa virusi vya Ebola katika eneo la Magharibi mwa nchi, hivyo kutokana na jografia iliyopo kati ya taifa hilo na Tanzania, taadhari inasisitizwa zaidi ili kuendelea kuwa na jamii salama.

"Tunajulikana kama timu ya wananchi. Falsafa yetu ni kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi,kutokana na kuwa karibu na jamii kwa kurejesha kwa jamii hilo limewashawishi UNICEF kufanya kazi na sisi kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa jamii.

“Sisi kazi yetu ya mpira tunafanya kazi na mashabiki kwa kuwapa burudani, hivyo wakiwa na afya inakuwa ni rahisi kwetu kuendelea kuwapa burudani jambo ambalo tunalifanya kwa sasa.

"Tunaunga mkono juhudi za Serikali kwenye kupambana na Corona pamoja na kutoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya Ebola.Tunashirikiana na UNICEF ili kila mwanachama, mpenzi na mshabiki wa Young Africans SC na vilabu vingine apate maarifa na uelewa kuhusu chanjo ya UVIKO-19,”amesema Rais Mhandisi Said.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Yanga SC, Andre Mtine amesema hii ni siku ya kihistoria kwa klabu hiyo kuingia mkataba mkubwa na shirika kubwa duniani.

Hii ni kwa mara ya kwanza katika historia kwa vilabu vya Afrika Mashariki kuingia mkataba wa miezi sita na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) unaolenga kuongeza uelewa kwa umma kuhusu chanjo ya UVIKO-19 na elimu kuhusu virusi vya Ebola.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNICEF, Bi,Fatimata Balandi amesema kuwa, wanafurahi kufanya kazi na Yanga SC kwa ajili ya kufikisha elimu kwa jamii.

"Yanga SC imetuonesha umuhimu wa michezo kwenye kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya, ushirikiano wetu utasaidia zaidi ya mashabiki milioni 25 wa soka nchini Tanzania kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo ya UVIKO-19 na virusi vya Ebola ili waweze kujilinda,"amesema Bi.Baladi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news