BRELA, ARIPO yawapiga msasa wadau

NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO) wametoa mafunzo kwa wadau juu ya uwasilishaji wa maombi kwa njia ya mtandao wa ARIPO.
Akifungua mafunzo hayo Novemba 8, 2022 katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu, Bw. Seka Kasera amesema mafunzo hayo kuhusu mfumo wa kisheria na wa kitaasisi wa Miliki Ubunifu yanalenga kuwawezesha washiriki na wadau ambao ni mawakala kutumia mfumo huo bila ya kupata changamoto yoyote.
"Lengo ni kuwafikia wadau ambao ni mawakala na watumiaji wa mfumo kwa kuwapatia elimu kuhusu mfumo wa kisheria na wa kitaasisi wa Miliki Ubunifu,"amefafanua Bw. Kasera.

Bw. Kasera amesema zoezi hili ni moja ya mkakati wa kuondoa na kupunguza urasimu wa uwepo wa watu wa kati (VISHOKA) wanaokwamisha taratibu za upatikanaji wa hataza kwa wafanyabishara.
Kwa upande wake Msajili Msaidizi Mkuu kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa wadau ambao ni mawakala na watumiaji wa mfumo wa Miliki Ubunifu nchini, kwa kusambaza elimu hiyo kwa wananchi wengine lakini pia kupunguza kero mbalimbali na gharama za utoaji wa hataza, suala ambalo mara kwa mara Serikali imekuwa ikilipigia kelele kwa nguvu zote.
Bi. Mhando amesema mpango huu wa mafunzo umezingatia umuhimu wa wadau ambao ni mawakala kuwa karibu na wafanyabiashara, kwa kutoa huduma bora, saidizi na elimishi ili kipato chao kiongezeke na hatimaye Serikali kupata kodi na uchumi wa nchi kukua na kuimarika.
Aidha, Mkuu wa Uchakataji maombi kutoka ARIPO Harare, Zimbabwe, Bw. Charles Pundo akiwasilisha mada kuhusu taratibu na hatua za kusajili Alama za Biashara na Huduma kupitia mfumo wa ARIPO, ametoa rai kwa wadau kujitokeza kwa wingi ili kutumia vyema fursa ya kuomba maombi mapya kwa njia ya mtandao.Mafunzo hayo ya siku tatu yatahitimishwa Novemba 10, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news