HATUWEZI KUMTUPA KAMA MPAGANI-II

NA ADELADIUS MAKWEGA

KATIKA matini iliyotangulia msomaji wangu nilikusimulia maisha ya Kingunge Ngombare Mwiru tangu anazikwa kikristo na maisha yake ya utoto.

Monsinyori Mbiku ambaye na yeye ni marehemu kwa sasa alinukuliwa akisema kuwa Kingunge wakati wa uhai wake alikuwa na mke wake aliyefahamika kama Peras Kingunge aliyefunga naye ndoa kanisani.
Je Kingunge alikuwa akiingia Ukristo na kutoka? “Alipopata mchumba mkatoliki binti huyu akataka kufunga ndoa ya kikatoliki, Kingunge alikataa, akaamuru kufunga ndoa bomani. Kweli wakafunga ndoa ya bomani, lakini Peras akaenda kwa Kadinali Lauriani Rugambwa wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam wakati huo, akamueleza kuwa mume wake kwa ndoa ya bomani amekataa kufunga ndoa ya Kikristo kwenye Kanisa Katoliki naye anaogopa kutengwa na Kanisa anafanyaje? ”

Kardinali Rugambwa akakabidhiwa malalamiko hayo, mwanakwetu inakuwaje? Kadinali huyo akaamua amuite Kingunge wazungumze.

Kingunge aliitikia wito huo alipofika Kadinali akamuuliza Kingunge wewe si mkristo? Kwa nini unafunga ndoa bomani? Huyu mkeo tunamtenga na kanisa. Kingunge akabaki na msimamo wake akisema yeye hana imani ya Mungu, kwa nini afunge ndoa kanisani?.

Kingunge aliombwa afunge ndoa kanisani kwa ndoa mseto kama anampenda mkewe ili abaki na dini yake.

Kingunge kwa kuwa na mapenzi na Peras alikubali kufunga ndoa kwa siri bila watu. Kadinali Rugambwa akakubaliana na hilo na ndoa ikafungwa ikiwa na watu watano tu; Kingunge, Peras wasimamizi wawili na Kadinali Rugambwa katika misa huko Kurasini katika nyumba ya makazi ya Wabenediktini. Misa ilipokwisha Kingunge alikwenda kazini na mkewe kurudi nyumbani na jioni walifanya sherehe fupi.

Marehemu Monsinyori Mbiku alisema kuwa mahusiano ya Kingunge na kanisa yalikuwa mazuri sana kwa kuwa katika nyakati fulani kule Goba kwenye Kigango cha Bikira Maria Mama wa Huruma Tanki Bovu wakati huo Hayati Kingunge alilitoa kama zawadi eneo lake lijengwe kanisa na mwenyewe alisema maneno haya,

“Mtakapomaliza kujenga kanisa nitakuwa mkristo wa kwanza kuingia katika hilo kanisa hilo.”

Baadaye walipoanza harakati za ujenzi eneo lilionekana dogo wakataka kuongeza nafasi, wakamtuma Msinyori Mbiku akamwombe awaongezee eneo, Kingunge akakubali kuwapatia kwa kuwauzia kwa bei ya chini.

Mwanakwetu hayo yote yalikuwa ni maelezo ya nyuma kabla ya kifo chake, yanathibitisha kuwa Kingunge alikuwa mtoro wa kusali, lakini matendo yake kiutu aliyafanya kwa kanisa na viongozi wake. Je hayo ndiyo yaliyosaidia Kanisa Katoliki kumpa huduma za kiroho?.

Marehemu Msinyoro Mbiku alisimulia kuwa baada ya kumzika mke wa Kingunge (Peras Kingunge) Kingunge na yeye alikuwa mgonjwa, alizidiwa na kurudishwa hospitali. Alipokuwa hospitali alizidiwa akazimia.

Ndipo wakamuita Padri Mbiku kama mwanafamilia na kiongozi wa kiroho alipofika hapo aliona mgonjwa yu mahututi hawezi kuzungumza.

“Nikasema mimi nitampatia huduma za kiroho ya sakramenti ya upako wa wagonjwa kwa sababu yeye ni mkristo maana miaka kadhaa iliyopita nilizungumza naye nikamuuliza wewe si mkristo? Akasema, ‘Mimi ni mkristo lakini bado ninajiuliza kama kuna Mungu kweli. Hilo tu ndilo nagombana nalo maana falsafa yangu inataka kuhakikisha kama kweli kuna Mungu.’ Nilimuliza huwezi kurudia ukristo wako ? Akasema anaweza lakini siyo sasa. Nilipoona amezimia nikakumbuka maneno yake, ‘Nitaamini lakini siyo sasa.’ Ndipo nikampatia huduma za kiroho, nikiamini ndiyo muda wake. Nilipomaliza nikawaambia wauguzi kuwa naondoka lakini akizinduka naomba mniite. Alipozinduka akawa yupo kawaida, wauguzi wakamueleza nilichofanya. Akauliza niko wapi akaamuru niitwe. Wakaja kwangu kunichukua.” Alieleza marehemu Padri Mbiku.

Nikamwambia una lolote tuzungumze? Akawasihi wahudumu wote watoke, abaki na mimi na nesi mmoja ,’‘Maana naumwa hivyo lazima awepo mmoja kwa dharura.’ Nikamueleza nilichokifanya, akaniambia, ‘Monsinyori umefanya vizuri sana na ninakushukuru kwa ulichofanya. Asante sana. Nikamwambia sasa tumalize kabisa urudi kwenye imani. Akasema Monsinyori ngoja nikueleze kilichonifanya hivi. Mimi nilikwenda Urusi, kule nilikaa miaka mingi nikisoma nikakutana na wakomunisti nikajifunza falsafa kuhusu Mungu yupo au hayupo.

“Wakomunisti wakasema hakuna Mungu. Mimi niliwakatalia nikawaambia nihakikisheni kuwa Mungu hayupo. Wakashindwa kunihakikishia. Nao wakanilazimisha kuwahakikishia kuwa Mungu yupo? Nami nikashindwa kuwahakikishia. Ndiyo falsafa yangu na nikarudi katika hilo hadi sasa. Wala sisemi kuwa hakuna Mungu lakini falsafa yangu haijanipa jibu kwamba kuna Mungu. Ndiyo hiyo nahangaika nayo. Kama kuna yeyote anaweza kunihakikishia anisaidie kwamba kuna Mungu niko tayari hadi sasa kuwa Mkatoliki.”

Mwanakwetu hapo Kingunge Ngombare Mwiru yu hospitalini kando yu muunguzi mmoja na Padri Mbiku tu hoja ikiwa kwa Padri Mbiku kumuhakikishia ndugu yake hilo la uwepo wa Mungu.

“Nikakumbuka maandishi ya Mtakatifu Anselmo, alitamka ‘Naelewa akilini mwangu ili niamini’, nami (Monsinyori) nikamwambia amini ili uelewe. Nikamwambia sasa kama una imani jaribu kuelewa uamini. Akasema hapana huko siko.Tena nilipata sakramenti zote za kanisa kasoro upadri. Kama unaweza kunihakikishia niambie ili akili ijue. Akili haijui ndiyo maana nahangaika. Kwa bahati mbaya katika mazungumzo haya Kingunge akaanza kuchoka na kuzidiwa, muuguzi akasema huyu amechoka.”

Kingunge akasema amefurahia upako wa wagonjwa yuko radhi kurudi kwenye imani Katoliki akamuomba aje tena kumueleza aelewe. Sina shaka na imani Katoliki. Falsafa tu inanisumbua. “Monsinyori mimi nakushukuru sana ulimzika mama yangu mzazi 1973 mwaka mmoja wa upadri wako pale Msimbazi, tena umemzika na mke wangu .”

Monsinyori alipokuwa analisimulia hayo alisema bayana kuwa alitamani siku ile kusema kuwa nitakuzika na wewe, lakini hilo hakulitamka. Baadaye mwankwetu Kingunge Ngombare Mwiru alifariki dunia

Alijulishwa Askofu Euzebius Nzigilwa kila hatua ya maisha ya ndugu huyu na mawasiliano yalifanywa kwa maaskofu wengine, baadaye ikaamuliwa kuwa kwa heshima ya mkewe na watoto wake waliokuwa wanamuombea abadilike, kwa heshima aliyokuwa anaonesha kwa kanisa, maana hakuwa mpinzani wa imani tusimtupe tu.

“Hatuwezi kumpeleka kanisani kwa misa ya mazishi maana alikuwa haendi kanisani na hatuwezi kumtupa kama mpagani kabisa, ikaamuliwa katekista afanye ibada kwenye maziko hayo.”

Mwanakwetu nilipoisoma nyaraka hiyo sasa nilielewa kwa nini Kingunge alizikwa namna ile na leo ndiyo nikaamua niisimulie nyaraka ile kama sehemu ya matini zangu mbili.

(NB Monsinyori /Mosinyo ni mtu anayefanya kazi katika ofisi ya Askofu, akitekeleza majukumu ya Kiaskofu japo hajafikia daraja hilo).

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news