MAJALIWA JACKSON HEKO SANA:Kijana kapata kazi, bidii na wema unalipa

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 7, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana Majaliwa Jackson aliyeona ndege ikianguka na kuamua kwenda kutoa msaada wa uokoaji akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na aingizwe katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili apate mafunzo zaidi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo wakati akiongoza wananchi kuaga miili ya watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege ya shirika la ndege la Precision Air katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Ajali ya ndege hiyo aina ya ATR 42-500 yenye namba za usajili 5H-PWF iliyotokea Novemba 6, 2022 asubuhi wakati ikijaribu kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba ikiwa na watu 43 wakiwemo abiria 39, marubani wawili na wahudumu wawili.

Waziri Mkuu amesema, taarifa za uokoaji zinaonesha kuwa watu waliookolewa ni 24 wakiwemo abiria 22 na wahudumu wa ndege wawili na waliopoteza maisha ni watu 19 wakiwemo abiria 17 na marubani wawili. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,katika safari ya maisha kuna siri nyingi za ajabu, endelea;

1. Tupo kufa kufaana,
Kijana tunamuona,
Amefanya ya maana,
Majeruhi kuwaona,
Kuokoa kapigana,
Ni wengi waliopona,
Wengi tumeshaagana
Kijana kapata kazi.

2. Kweli lijituma sana,
Tena kwa bidii sana,
Wengi waliomuona,
Na kumpongeza sana,
Ni ajali mbaya sana,
Akili zavurugana,
Tunamuona kijana,
Yeye amepata kazi.

3. Majaliwa twanuona,
Mwenzake wameshikana,
Habari tunaiona,
Neema yaambatana,
Huko kufa kufaana,
Mambo yake yananona,
Jeshini tutamuona,
Ndiyo amepata kazi.

4. Maisha ajabu sana,
Mwanga tunavyouona,
Si pande kupigiana,
Kwingine tunavyoona,
Ni Mungu tunamuona,
Mtu wake amuona,
Kwa kuwajibika sana,
Sasa amepata kazi.

5. Na tutamuimba sana,
Ushujaa wa kijana,
Ndege alipoiona,
Ziwani imejibana,
Kena kujituma sana,
Nao kusaidiana,
Wamekufa wameoona,
Yeye amepata kazi.

6. Hili somo zuri sana,
Wema ni mzuri sana,
Bila.taka kulipana,
Huo uungwana sana,
Hadi Mungu akuona,
Watu wengi wakuona,
Na kukupongeza sana,
Hadi unapata kazi.

7. Pongezi ni nyingi sana,
Hilo jambo kuliona,
Kumtambua kijana,
Kazi yake nzuri sana,
Hadi Rais kuona,
Kwamba anafaa sana,
Naye tuzidi muona,
Jeshini afanye kazi.

8. Majaliwa heko sana,
Mungu wako kakuona,
Huko kufa kufaana,
Waziwazi tunaona,
Kweli tunalia sana,
Majonzi ni mengi sana,
Lakini kwako kijana,
Ndiyo umepata kazi.

9. Tunasikitika sana,
Maisha wale hawana,
Ndugu wote pole sana,
Taifa mmeliona,
Sote tumeguswa sana,
Haya tuliyoyaona,
Lakini kwake kijana,
Ndiyo amepata kazi.

10. Majeruhi pole sana,
Na tena hongera sana,
Ajali ndege twaona,
Kupona nadra sana,
Nyie Mungu kawaona,
Hebu mshukuru sana,
Ajali kwake kijana,
Ndiyo amepata kazi.

11. Tutafurahi kuona,
Majeruhi mkipona,
Turudie kuwaona,
Mnawajibika sana,
Wengineo chonde sana,
Wivu msijekuona,
Mmesaidia sana,
Yeye amepata kazi.

12. Wahusika wengi sana,
Na mmepambana sana,
Wote tunaowaona,
Nguvi yenu kubwa sana,
Tunawapongeza sana,
Wema wenu bomba sana,
Na mmechangia sana,
Kijana kapata kazi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news