HAWA TEMBO WARRIORS, WANG’ARISHA TANZANIA

NA LWAGA MWAMBANDE

MIONGONI mwetu katika jamii, tumekuwa na kasumba ya kufanya vitu ilimradi kusukuma siku au tunaweza kusema, ninafanya jambo hili siku iende tu.

Uvivu, huo umekuwa moja wapo ya sababu inayochangia wengi wetu licha ya akili, utimilifu wa viungo na nguvu tulizonazo hatusongi mbele kimaisha, badala yake tunajikuta tunaendelea kuwa tegemezi na kuelekeza lawama kwa familia kama si kwa Serikali.

Tambua,bidii, maarifa, nguvu na akili vikitumika vema lazima usonge mbele kimaisha. Turejee kwa Watanzania wenzetu ambao wana ulemavu wa viungo ambao siku za karibuni wameishangaza Dunia kupitia soka, si wengine bali ni Tembo Warriors ambao walifanya maajabu katika Kombe la Dunia.

Ndugu hawa wametupa funzo kuwa, kuwa na ulemavu si kigezo cha kukwama kimaisha, kwani unaweza kufanya zaidi ya yule aliyekamilika. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, bidii inalipa na tayari vijana wa Tembo Warriors mambo yao yametiki, endelea;

1:Tembo Warriors sita, watacheza Uturuki,
Ni timu wameshapata, mambo yao yametiki,
Hilo shavu wamepata, yao mikiki mikiki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

2:Wachezaji wa kulipwa, Ulaya ya Uturuki,
Hawaendi kwa kukopwa, huko wanapata keki,
Mshahara tipwatipwa, zitanona zao cheki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

3:Ni wawakilishi wetu, duniani walitiki,
Sasa ligi za wenzetu, tayari wamewalaiki,
Hiyo sifa kubwa kwetu, na wataleta Malaki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

4:Na waliotangulia, huko huko Uturuki,
Kwa sasa wamefikia, toa tisini kwa laki,
Sifa kubwa Tanzania, tunatamba Uturuki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

5:Ni wa timu ya taifa, soka wenda Uturuki,
Waongeze maarifa, ya soka kulimiliki,
Wakija tupate sifa, michezo tukishiriki,
Hawa Tembo Warriors, Wang’arisha Tanzania.

6:Tukumbuke hii timu, mefanya yenye mantiki,
Jinsi ilivyojihimu, mpira kuumiliki,
Kombe dunia kutimu, kwa kweli tuliwacheki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

7:Ni robo fainali, walikokwaa kisiki,
Hiyo ni hatua kali, kweli tumewaafiki,
Sasa twaona kibali, hao wenda Uturuki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

8:Hongera kwa chama chao, kazi yenu twaafiki,
Wizara kwa kazi yao, kuwatunza hawachoki,
Imebaki kazi kwao, huku walete Malaki,
Hawa Tembo Warriors, wang’arisha Tanzania.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news