NI SIMBA QUEENS, SIMBA QUEENS: BENDERA YA TANZANIA INAPEPEA

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 5, 2022 Kikosi cha Simba Queens kilitinga Nusu Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuifunga Green Buffaloes kutoka Zambia katika mchezo wa mwisho wa Kundi A. Ni katika mtanange wa nguvu uliopigwa katika dimba la Marrakech jijini Marrakech,Morocco.

Katika mchezo huo, Djafar alipoteza nafasi ya wazi dakika ya 43 baada ya shuti lake la chini chini kutoka nje kidogo ya lango akiwa anatazamana na mlinda mlango baada ya kupokea pasi ya Opa Clement.

Aidha,kipindi cha pili Simba Queens waliongeza kasi na kuliandama lango la Buffalos ambapo dakika ya 64, Djafar alitupia bao la kwanza kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Fatuma Issa.

Pia nahodha Opa Clement alitupia bao la pili dakika ya 79 baada ya kupokea pasi ndefu ya mpira wa kutengwa iliyopigwa na mlinzi wa kati Daniela Kanyanya.

Kwa matokeo hayo, msahiri wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, Simba inaendelea kuibeba Tanzania, kikubwa ni kuwaombea kila la heri, endelea;


1:Bendera inapepea, ya taifa Tanzania,
Simba inaendelea, kuibeba Tanzania,
Wengi tunachekelea, hapa tulipofikia,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

2:Walianza kwa kusua, tukajisikitikia,
Kisha wakajinasua, ushindi kujipatia,
Sasa wamekwishakua, inang’aa Tanzania,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

3:Haijapata tokea, hapa kwetu Tanzania,
Timu zetu kusogea, Simba ilipofikia,
Pongezi zaendelea, kotekote Tanzania,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

4:Sote twaangalia, wang’arisha Tanzania,
Mpira watupigia, twaona twafurahia,
Raha tunaipitia, hapa tulipofikia,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

5:Pongezi kwa wachezaji, waibeba Tanzania,
Makocha wa wachezaji, kazi wanatufanyia,
Uongozi kwa mtaji, huo mmetupatia,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

6:Hapo mlipofikia, Simba Queens Tanzania,
Deni mmeshalipitia, hata kupitilizia,
Rekodi zinaingia, mpya hapa Tanzania,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

7:Kwenye michezo mitatu, mnatuwakilishia,
Tuna wachezaji wetu, ubora wamefikia,
Hiyo pia sifa kwetu, inakuja Tanzania,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

8:Hivi nani kama Opah, nahodha tunaringia,
Walinzi wanamkwepa, anavyowafanyizia,
Kweli Opah analipa, sote twamfurahia,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

9:Asha Jafari jamani, bao alotufungia,
Tamu laenda moyoni, vile tumefurahia,
Kweli twatamba mjini, hii yetu Tanzania,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

10:Hapo tulipofikia, mbele tunaangalia,
Heri tunawatakia, tuzidi kufurahia,
Fainali kuingia, tutaruka nakwambia,
Simba Queens Simba Queens, Nusu Fainali CAF.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments