HUU USHIRIKIANO, WENGINE WAFUATIE

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA Mosi, 2022 Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameyataka mashirika ya Posta Tanzania na Kenya kuhakikisha wanafanya biashara ya usafirishaji kwa njia ya kidigitali zenye kukidhi vigezo vya kimataifa.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew (kulia) kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akikabidhi mfuko wa kufungia barua na vifurushi vya Kenya kwa Postamasta Mkuu wa Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo.

Lengo likiwa ni kuwavutia wananchi wa nchi hizo kufanya biashara na mashirika hayo ambayo yanategemewa kutoa huduma za haraka, bora na kwa ufanisi zaidi.

Ameyasema hayo jijini Arusha katika hafla ya uzinduzi wa biashara ya kuvuka mpaka kwa njia ya kidigitali kati ya Tanzania na Kenya iliyofanyika katika mpaka wa Namanga.

Uwepo wa biashara hiyo kwa nchi hizo unatarajiwa kubadilisha muundo mzima wa kidigital katika kufanya usafirishaji wa vifurushi hivyo kwa wateja wake na kuwafikia ndani ya muda ikiwemo kuokoa gharama zilizokuwepo hapo awali.

Pia uwepo wa mfumo huo utaongeza fursa za ajira kwa vijana walio wengi,kwani kwa kufanya hivyo wanaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,Posta wameanzisha, wengine wafuatie;

1:Afrika Mashariki, ile tunayotamani,
Aste aste tiki, twashuhudia machoni,
Ni mambo yenye mantiki, Tanzania Kenya ndani,
Posta wameanzisha, wengine wafuatie.

2:Huu ushirikiano, umeshatiwa saini,
Tena ni mzuri mno, watukumbusha zamani,
Jumuiya ile nono, livyotamba duniani,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

3:Posta za nchi mbili, kwenye jumuiya ndani,
Pamoja wamejadili, kukabili ushindani,
Wameafiki kamili, ushirika ni madini,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

4:Mashirika nchi mbili, kibiashara makini,
Umoja kuwa wawili, kukabili ushindani,
Yameshika nchi mbili, mmoja utamaduni,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

5:Jumuiya yetu hii, Zaidi ya ishirini,
Miaka tuna bidii, kwa biashara za ndani,
Posta wameshatii, waenda Zaidi ndani,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

6:Tutegemee mazuri, ajira nyingi kazini,
Na pia huduma nzuri, ugenini na nchini,
Tuzidi ona fahari, mambo haya ya madini,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

7:Mizigo kimataifa, inayokuja nchini,
Wamefanya maarifa, wa vituo vya njiani,
Wataziba zote nyufa, uchelewaji njiani,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

8:Zifike zetu pongezi, Posta yetu nchini,
Jinsi linafanya kazi, na mengine duniani,
Linajitokeza wazi, kwa mpya utamaduni,
Posta wameanzisha, wengine waendelee.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments